Pichani Meneja wa mawasiliano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudencia Simwanza akionyesha mojawapo ya dawa za kuongeza matako na matiti kwenye viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Nyerere (DITF), dawa hizo zimeelezwa kuwa na athari zinazosababisha kansa.
Wakati huo huo TFDA imewatahadharisha wanawake wanaotumia vipodozi vya kuongeza makalio na matiti kwamba wanaweza kupata madhara ya figo, ubongo na kansa ya ngozi.
Mkaguzi wa dawa vipodozi na vifaa vya tiba wa TFDA Kissa Mwamwita alisema kumekuwa na wimbi kubwa la wanawake wanaotumia vipodozi hivyo ambavyo havijasajiliwa na mamlaka hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mwamwita alisema vipodozi hivyo vimekuwa vikiingizwa nchini na kuuzwa kwa kificho huku ikidaiwa kuwa wateja wake wakubwa ni wanafunzi wa sekondari na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
Mwamwita aliwataka wanawake wanaotumia vipodozi kuwa makini wakati wanaponunua vipodozi kwa kuangalia kama vimesajiliwa kwani vipo vipodozi vinavyouzwa kwa kificho.
“Matumizi ya vipodozi hivyo vinavyoongeza ukubwa wa makalio na matiti ni hatari kwa afya na pia yanawaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya saratani,” alisema Mwamwita.
Alisema watumiaji wa vipodozi wanatakiwa kuwa makini wanapotaka kununua bidhaa hizo ili kuepuka kununua vipodozi vyenye viambata vya sumu.
Hata hivyo TFDA imetoa tahadhari kwa wananchi wanaoendelea kutumia vipodozi vyenye viambata vya sumu zikiwemo ‘losheni’ kuacha kutumia kwa kuwa kiafya vina madhara makubwa.
Mwamwita alitaja baadhi ya vipodozi vyenye viambata kuwa ni Chloqinone,Chloroform na Mercury Compound.
Comments