Saturday, September 20, 2008

Rais kwenda Marekani

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete anaondoka nchini leo (Jumamosi, Septemba 20, 2008) kwenda New York, Marekani, ambako atahudhuria na kuhutubia kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).

Rais amepangiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumanne ijayo, Septemba 23, 2008 katika nafasi yake pia kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Mbali na kuhutubia Baraza Kuu, Rais Kikwete amepangiwa kuhudhuria mikutano mingine muhimu kuanzia ule ambao utaangalia Mahitaji ya Maendeleo ya Afrika. Mkutano huo, utajadili ahadi za nchi tajiri kwa Afrika na Maendeleo ya Bara hilo, na kuona ahadi hizo zinatekelezwa namna gani.

Rais pia atahutubia kikao cha ufunguzi cha viongozi ambao watajadili maendeleo ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s). Baada ya kuwa amehutubia kikao hicho, Rais atashiriki katika mijadala kuhusu afya ya Mama na Mtoto, na pia mjadala kuhusu ugonjwa wa Malaria, masuala yote mawili yakiwa sehemu muhimu ya MDG’s.

Ijumaa, Septemba 26, Rais atakwenda mjini Washington, ambako atatoa hotuba muhimu ya ufunguzi kwenye Kikao cha Mwaka cha Wabunge Wenye Asili ya Afrika katika Bunge la Marekani, na pia kuhutubia mkutano wa viongozi wa shughuli za biashara katika Marekani.

Mbali na mikutano ambayo amepangiwa kuhutubia ama kushiriki, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wengi wa shughuli za kisiasa, kibiashara na kiuchumi duniani na katika Marekani.

Miongoni mwa viongozi ambao Rais Kikwete atakutana nao na kufanya mazungumzo nao ni pamoja na Rais wa Iran, Mheshimiwa Ahmedinajad; Katibu Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Mheshimiwa Javier Solana; na mfanyabiashara maarufu duniani wa shughuli za kompyuta na teknolojia ya mawasiliano, Bill Gates.

Rais Kikwete pia atakutana na Waziri Mkuu wa Denmark, Mheshimiwa Anders Fogh Rasmussen; na Katibu Mkuu wa Shirika la Kazi Dunia (ILO), Juan Somavia.

Rais Kikwete pia atafanya kikao cha pamoja kati yake, Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki Moon na Makamu wa Rais wa Sudan, Ustaz. Ali Osman kuzungumzia mgogoro wa eneo la Darfur nchini Sudan.

Wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika Sudan mwanzoni mwa mwezi huu, Mwenyekiti huyo wa AU, alimwahidi Rais Omar El Bashir wa Sudan kuwa angefanya kikao kati yake, Katibu Mkuu wa UN, na mwakilishi wa Sudan kuhusu hali ya Darfur wakati wa Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu.

Kikao hicho kitaangalia jinsi gani ya kuharakisha zoezi la kupeleka askari wa kulinda amani wa UN na AU katika Darfur, na pia jinsi ya kuahirisha, kwa angalau mwaka mmoja, hati ya kukamatwa kwa Rais Bashir iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uharifu (ICC).

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.



20 Septemba, 2008

No comments: