Vaileth malkia wa Miss Utalii Tanzania
Na Jessca Nangawe
MREMBO Vaileth Timoth kutoka Dar es salaam jana alifanikiwa kutwaa taji la Miss utalii baada ya kuwabwaga wenzake 20 na kunyakuwa gari mpya aina ya Nissan Premira yenye thamani ya shilingi mil.15 katika kinyang'anyiro cha kumsaka miss utalii Tanzania lililofanyika kwenye ukumbi wa New World Cinema, Mwenge.
Shindano hilo lililokuwa la kusisimua na lenye ushindani wa hali ya juu jumla ya warembo 21 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania walipanda jukwaani katika mavazi tofauti tofauti yaliyokua yakiutangaza utalii na utamaduni wa Tanzania.
Katika hatua ya kwanza warembo kumi walifanikiwa kuingia katika hatua ya kumi bora ambapo kila mmoja alitakiwa kuelezea utalii wa Tanzania kwa jinsi anavyofahamu.
Waliofanikiwa kuingia katika hatua ya tano bora ni Zulfa Hahya (Kagera), Elizabeth Kilya(Kilimanjaro),Evalyne Julius (Manyara), Aneth Kanora (Arusha) na Vaileth Timoth Dar es salaam.
Aidha mshiriki kutoka Mkoa wa Mara, Josina Henry aliibuka Miss Vipaji mara baada ya kuonyesha umahiri mkubwa katika kuimba na kuonyesha uhalisia wa utamaduni wa Kitanzania katika shindano lililofanyika mkoani Morogoro wiki iliyopita na kujinyakulia kitita cha shilingi laki 5.
Zawadi kwa mshindi wa pili alikuwa ni Shs mil.2 ilikwenda kwa Aneth Kanora (Arusha) , wa tatu mil 1.5 Evalyne Julius (Manyara) wa nne Elizabeth Kilya (Kilimanjaro) na wa tano Zulfa Yahya (Kagera) pamoja na Miss vipaji waliondoka na laki 5 kila mmoja.
Naye Waziri wa Maliasili na utalii Shamsa Mwangunga ambae alikua mgeni rasmi katika shindano hilo alimtaka mrembo huyo kuiwakilisha Tanzania vema kwa upande wa mambo ya utalii katika mashindano ya Dunia.
"Tumekuwa na warembo ambao wamekuwa wakiwakilisha nchi kwenye mashindano ya dunia sasa ni wakati wako kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania,"Alisema Mwangunga.
Aidha Waziri alisisitiza waandaaji wa shindano hilo kutoa zawadi kwa wakati na ili walikusudia kwa nia ya kurudisha imani ya washiriki na wazazi kwa ujumla.
Comments