Morogoro – Baadhi ya wakazi wa eneo la Kihonda Mbuyuni, Manispaa ya Morogoro, wameanza kutumia makuti na kuni kama mbadala wa nishati ya kupikia baada ya bei ya mkaa kupanda kutoka Sh 15,000 hadi Sh 20,000 kwa gunia.
Mabadiliko haya yamewalazimu wananchi, hasa wa kipato cha chini, kutafuta njia mbadala za kupikia kutokana na ugumu wa kumudu gharama za mkaa. Akizungumza na mwandishi wetu, mkazi mmoja wa Kihonda Mbuyuni alisema kuwa kwa sasa, kuni na makuti vimekuwa msaada mkubwa kwa familia nyingi ambazo haziwezi kumudu gharama za mkaa zinazozidi kupanda kila siku.
“Mwanzo tulikuwa tunanunua gunia moja la mkaa kwa Sh 15,000, lakini sasa linauzwa Sh 20,000. Hali imekuwa ngumu sana, ndiyo maana tumelazimika kutumia makuti na kuni kwa ajili ya kupikia,” alisema mkazi huyo.
Wauzaji wa mkaa katika soko la Kihonda wanasema kuwa kupanda kwa bei ya mkaa kunatokana na gharama kubwa za usafirishaji na kupungua kwa upatikanaji wa nishati hiyo kutokana na kanuni zinazodhibiti ukataji miti kiholela.
“Hivi sasa tunanunua mkaa kwa bei ya juu kutoka kwa wasambazaji, na gharama za usafirishaji nazo zimepanda. Hili limechangia ongezeko la bei tunaloliona sasa,” alisema mmoja wa wauzaji wa mkaa.
Wataalamu wa mazingira wameeleza kuwa ongezeko la bei ya mkaa linaweza kuwa fursa ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama gesi na umeme, lakini changamoto kubwa inabaki kuwa gharama na upatikanaji wa nishati hizo kwa wananchi wa kipato cha chini.
Serikali kwa upande wake imekuwa ikihamasisha matumizi ya nishati safi kama gesi ili kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni, huku ikiendelea kudhibiti ukataji miti kiholela unaochangia uharibifu wa mazingira.
Kwa sasa, wakazi wa Kihonda Mbuyuni na maeneo mengine nchini wanaendelea kuhangaika na changamoto ya gharama za nishati ya kupikia, huku wakiangalia mbinu mbadala za kukabiliana na hali hiyo. Picha ya Juma Ahmadi.
No comments:
Post a Comment