Ilikuwa siku, wiki mwezi na miezi na hatimaye miaka mitatu na miezi kadhaa ilikwisha, Zephania Msendo alijikuta kuwa mtu huru tena juzi baada ya kumaliza adhabu yake ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu.
Aliachiwa huru kutoka gereza la Mkuza lililo Kibaha mkoani Pwani.
Musendo ni mwandishi mwandamizi ambaye amepitia vyombo mbalimbali vya habari, mara ya mwisho akiwa analiongoza gazeti la Family Mirror akiwa mhariri mkuu.
Lakini bidii yake ya kazi na ujuzi aliokuwa nao ulizimwa ghafla baada ya Hakimu wa Mahakama ya Kisutu kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela kwa madai ya kula rushwa ya Sh 100,000 baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCB) kumshtaki.
“Imeathiri sana maisha yangu, imeharibu familia yangu na nimepata hasara kwani kipato kimesimama kwa muda wote na mipango yangu imeparanganyika,” anasema Musendo katika mahojiano maalum na gazeti la Mwananchi jana.
Msendo, ambaye kwa sasa ameungana na familia yake nyumbani kwake Kawe jijini Dar es Salaam, anasema kuwa mipango yake kwa sasa ni kujiweka sawa, na kama akipata kazi atashukuru ili aweze kuisaidia tena familia yake akiwa kichwa cha familia. Imeandikwa na Mpoki Bukuku.
Comments