WAZIRI
wa zamani wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Jackson Makwetta
amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es
Salaam jana.
Taarifa
zilizopatikana jana na kuthibitishwa na mtoto wa marehemu, Tumwanuke
Makwetta zilisema kuwa marehemu alifariki jana jioni katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili jijini ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu.
Kabla
ya kuhamishiwa Muhimbili, mwanasiasa huyo mkongwe nchini, alifikishwa
Hospitali ya Lugalo wiki iliyopita baada ya hali yake kuwa mbaya
kutokana na maradhi ya moyo.
Mtoto
wa marehemu, Tumwanuke Makwetta aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa
taarifa zaidi kuhusu msiba wa mzee wao zitatolewa baadaye.
“Kwa
sasa siwezi kusema lolote kwa sababu ndiyo tunatoka hospitali kuelekea
nyumbani, taarifa zaidi nitakujulisha baadaye,” alisema.
Mtoto wa marehemu alisema kuwa baba yao alifariki jana jioni walipokwenda kumjulia hali.
Makwetta
alianza kuugua akiwa nyumbani kwake Njombe na akapelekwa kutibiwa
katika Hospitali ya Consolata ya Ikonda, wilayani Makete na baadaye wiki
iliyopita alihamishiwa katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam
baada ya kuzidiwa.
Muda mfupi kabla ya kifo chake, Rais Jakaya Kikwete alifika hospitalini hapo kumjulia hali.
Gazeti
hili lililokuwa hospitalini hapo lilishuhudia msafara wa Rais ukifika
hospitalini hapo na kuingia wodini na baadaye kuondoka.
Rais Kikwete alitumia fursa hiyo pia kuwapa pole wagonjwa wengine waliokuwa wakihudumiwa hospitalini hapo.
Wasifu
Alizaliwa
Juni 15, 1943. Alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka
1976-1980, mwaka 1982-83 alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Makwetta
pia aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na Chakula mwaka 1983-1987,
alibadilishwa wizara na kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
mwaka 1987-1989.
Marehemu
alishika wadhifa wa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi mwaka mmoja
kuanzia 1989-1990 na baadaye alihamishiwa Wizara ya Kilimo na Chakula
mwaka 1991-1992.
Pia amewahi kuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu mwaka 1995-1998.
Makwetta
amekuwa Mbunge wa Jimbo la Njombe Kaskazini tangu 1975 hadi 2005,
alipoenguliwa katika kura za maoni na aliyekuwa mgombea mpya wa CCM, Deo
Sanga.
Pia marehemu ni miongoni mwa mawaziri walioshika nyadhifa za uongozi katika Serikali ya Muungano katika awamu tatu;
Awamu
ya Kwanza ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Awamu ya
Pili ya Ali Hassan Mwinyi na Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa.
No comments:
Post a Comment