Kamanda
wa Polisi mkoani Tanga, Constatine Masawe, amethibitisha kutokea kwa
ajali iliyosababisha kifo cha Msanii, Sharo Milionea, aliyepata ajali
usiku wa kuamkia leo mida ya saa mbili usiku katika kijiji cha Lusanga,
Muheza mkoani Tanga.
*********************
MSANII
mahiri wa filamu na muziki wa Bongo Flava nchini, Hussein Mkiety
almaarufu, Sharo Milionea, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo majira
ya saa mbili jana usiku, kwa ajali ya gari katikati ya Kijiji cha
Lusanga na Maguzoni Songa, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga, Constatine Masawe,Sharo alikuwa peke yake garini wakati ajali hiyo ikitokea na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali Teule ya Muheza.
Kamanda Masawe alisema
Milionea, akiwa anaendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier akitokea
Dar es Salaam kwenda Muheza alipofika eneo hilo gari lake liliacha njia
na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake.
Hii ni ajali ya pili kati ya
alizowahi kupata msanii huyo, Sharo kwa mwaka huu baada ya Januari 5
kunusurika katika ajali ya basi alilokuwa amepanda la Taqwa likitokea
Burundi kuelekea Dar es Salaam kupinduka katika eneo la Mikese, Morogoro
saa mbili na nusu asubuhi.
Sharo ambaye alikuwa amekaa
kwenye siti ya mbele kabisa alipoteza simu tu katika ajali hiyo ambayo
ilijeruhi abiria wengine vibaya.
Kifo cha Sharo kinafuatia vifo
vya wasanii wengine wawili wa filamu nchini ndani ya wiki moja, Mlopelo
aliyetamba na kundi la Kaole na John Maganga aliyetamba na filamu
ya 'Mrembo Kikojozi' aliyocheza na Aunt Ezekiel.
Vifo hivyo vinakumbushia msiba wa Steven Kanumba, ambaye pia alifariki ghafla.
Sharo atakumbukwa kwa ubunifu
wake katika uigizaji akitoka kama mchekeshaji msafi tofauti na
wachekeshaji wengi waliomtangulia ambao waliamini vichekesho ni lazima
kuvaa kama katuni, kujaza nguo tumboni ili kuonekana na matumbo makubwa
ama kujipaka masizi.
Akipendeza kwa mavazi nadhifu,
Sharo Milionea alipata umaarufu kwa msemo wake wa "kamata mwizi
meeen" na "Ooooh mamma!" huku akijipangusa mabega katika pozi za
kibrazameni.
Katika siku za karibuni
amekuwa akitawala vioo vya televisheni kutokana na kushiriki tangazo
la kampuni ya huduma za simu ya Airtel akiwa na mchekeshaji mkongwe King
Majuto, ambapo msemo wake mwingine wa "umebugi meen!" umetawala hasa
midomoni mwa watoto.
No comments:
Post a Comment