Wauguzi
katika hospitali ya Rufaa ya Maweni wakitoa namba kwa wagonjwa
waliojitokeza kuonana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya taifa ya
Mhimbili
Dk.
Vence (Katikati) akiwa katika chumba cha upasuaji kutoa huduma kwa
mmoja wa watoto ambao walifanyiwa upasuaji mapema leo (jana)
Daktari
Bingwa wa akina Mama Dk. Mrema (wapili kutoka kulia) akimsikiliza kwa
makini mmoja wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo kwa lengo la kutoa
ushauri wa tiba sahihi.
Na Grace Michael, Kigoma
JUMLA
ya wagonjwa 316 ndani ya siku mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Maweni
mkoani Kigoma wamefanikiwa kuonana na madaktari bingwa kutoka Hospitali
ya Taifa Muhimbili ambao wapo mkoani humo kwa mpango unaoendeshwa na
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mbali
na wagonjwa hao kuonana na madaktari hao, jumla ya wagonjwa 11 ndani ya
muda huo nao wamefanikiwa kufanyiwa upasuaji na madaktari hao hali
inayoonesha kuwepo uhitaji mkubwa wa madaktari katika mikoa ya pembezoni
ambayo miundombinu yake bado haijaimarika.
Hayo
yanafanyika katika Mkoa wa Kigoma ndani ya mpango wa NHIF ambao
ulizinduliwa mapema Aprili mwaka huu mkoani Lindi ambako nako timu ya
madaktari bingwa watatu waliweka kambi katika Hospitali ya Mkoa na
kufanikiwa kutoa huduma kwa mamia ya wananchi.
Katika
Hospitali ya Maweni, timu ya madaktari wanne kutoka Muhimbili ilianza
kazi rasmi jana (Jumatatu) na itakaa hospitalini hapo kwa muda wa siku
saba lengo ni kutumia wataalam hao kitaifa.
Wagonjwa
wanaonufaika na mpango huu ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya na wananchi kwa ujumla ambao wanapata huduma kupitia utaratibu wa
kawaida.
Wagonjwa
waliofanikiwa kujiandikisha kwa lengo la kupata huduma kutoka kwa
wataalam hao ni kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Kigoma ambapo
wanaeleza kuwa ni fursa ya kipekee kuipata.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi wagonjwa ambao wamepata huduma ambao
walifikishwa hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya waliushukuru Mfuko
kwa kuanzisha mpango huo ambao moja kwa moja unawagusa wananchi hasa wa
kipato cha chini.
Kwa
upande wa watumishi hospitalini hapo, wanasema kuwa wataitumia fursa hii
vyema hasa katika kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa madaktari hao
bingwa ili waweze kuboresha huduma zao kwa wagonjwa hata watakapobaki
wenyewe.
Idadi
ya wagonjwa inazidi kuongezeka kila kukicha hatua inayowalazimu
madaktari hao kufanya kazi kwa zaidi ya saa 15 bila ya kupumzika.
Akizungumzia
mwitikio huo, Naibu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Hamis
Mdee, alisema kuwa mwitikio huo ni faraja kwa Mfuko ambao lengo lake ni
kutoa huduma kwa Watanzania na kuhakikisha afya zao zinaimarika.
“Sisi
kama Mfuko tunaona faraja sana tunapoona wagonjwa wamefika hapa na
kupata huduma hizi ambazo pengine wasingeweza kuzipata hivyo tutaendelea
na mpango huu kwa kuwa unagusa moja kwa moja uhai wa wanachama wetu na
wananchi kwa ujumla,” alisema Mdee.
NHIF imeanzisha mpango huu na utatekelezwa katika mikoa mbalimbali ya pembezoni ikiwemo Rukwa, Katavi, Pwani, Lindi na Kigoma.
Comments