Monday, July 26, 2010

Sita kortini kwa wizi wa fedha kimtandao




MHASIBU wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Justuce Katiti na wenzake watano jana walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 10, likiwemo la kughushi na kujipatia Sh338.9 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Kufikishwa mahakamani kwa wtau hao ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa na mamlaka husika dhidi ya wizi wa kimafia wa mabilioni ya fedha ambao gazeti hili liliripoti katikati ya mwaka kuwa unafanyika kupitia taasisi mbalimbali za kifedha.
Wakili mwandamizi wa serikali, Fredrick Manyandahati, akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Aloyce Katemana, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Fortunatus Muganzi, Robert Mbetwa na Gidion Otullo ambao ni wafanyakazi wa benki ya NBC.
Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni mfanyakazi wa Barclays, Godwin Paulla na mfanyakazi wa kampuni ya Tourism Promotion Services (Tanzania) Limited, Joseph Kaplamai Rutto.
Manyanda alidai kuwa kati ya Septemba 29 na Oktoba 6, 2008 washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kuitapeli benki ya Baclays.
Alidai Septemba 29, 2008, kwa makusudi Godwin na Joseph walighushi nyaraka ya uhamisho wa fedha kwa njia ya mtandao (Request for Swift Tranfer form E. 17) wakijaribu kuonyesha kuwa kampuni ya Tourism Promotion Services (Tanzania) Limited imeomba Baclays kuilipa East Africa Procurement Services Limited Tanzania Sh338, 935,337.46 kama madai ya kuiuzia mahema na vifaa vya hoteli.
Wakili huyo wa serikali alidai washtakiwa hao waliwasilisha nyaraka hiyo Baclays na kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia ya udanganyifu wakionyesha East Africa Procurement Services imelipwa fedha hizo na Tourism Promotion Services kwa kuuziwa mahema na vifaa hivyo vya hoteli.
Ilidaiwa kuwa Septemba 30 mwaka huo, Katiti alimdanganya mwajiri wake kinyume na Sheria namba 11 ya mwaka 2006 ya Kupambana na Kuzuia Rushwa, kwa kuandaa taarifa potofu ya makusanyo ya fedha na kujaribu kuonyesha kuwa Tourism Promotion Services ilikuwa imelipa kodi ya Sh338.9 milioni kama ongezeko la thamani kwa mwezi Agosti.
Pia Katiti anadaiwa kughushi nyaraka nyingine Oktoba 6,2008 akionyesha kuwa kampuni hayo imelipa fedha hizo.
Manyanda alidai kuwa kati ya Septemba 29 na Oktoba 6, 2008 washtakiwa hao kwa pamoja walihamisha fedha haramu wakati wakijua kuwa chanzo chake ni kosa la jinai na kuzificha. Wanadaiwa kuzitoa fedha hizo kutoka akaunti namba 0121186000 iliyo CRDB kwenda akaunti namba 1065822 na 600283 za Baclays na nyingine namba 240603616 ya Benki ya Biashara ya Kenya (KCB).
Wote walikana mashtaka yote yanayowakabili na upande wa mashtaka uliomba kesi hiyo iahirishwe kwa sababu upelelezi upo katika hatua za mwisho na hakimu akaiahirisha hadi Agosti 9, huku washtakiwa wakinyimwa dhamana. Imeandikwa na Tausi Ally SOURCE: MWANANCHI

No comments: