Dk Betty Machangu akifafanua jambo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuzungumzia tuhuma za kukamatwa na Takukuru akigawa rushwa kwa ajili ya kura za maoni za Ubunge viti maalumu mkoa Kilimanjaro. (Picha na Daniel Mjema)
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
VITA dhidi ya rushwa ndani ya CCM vimezidi kushika kasi baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kumtia mbaroni mkuu wa wilaya ya Kasulu, Betty Machangu akigawa rushwa kwa wajumbe.
Machangu ambaye anawania Ubunge wa viti maalumu kupitia mkoa Kilimanjaro, alinaswa na maofisa wa Takukuru sambamba na viongozi waandamizi wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) ngazi ya mkoa na Wilaya.
Kamanda wa Takukuru mkoa Kilimanjaro,Alexander Budigila, alisema tukio la kukamatwa kwa Machangu na viongozi hao lilitokea juzi saa 1:00 usiku katika Nyumba ya kulala wageni ya Safari Resort iliyopo Manispaa ya Moshi.
Machangu alinaswa na maofisa wa Takukuru akiwa amejifungia katika chumba namba 24 pamoja na viongozi hao ambapo baada ya maofisa hao kuingia ndani, walikuta vipeperushi vikiwa vimefichwa kwenye tanki la choo.
Pia katika chumba hicho, maofisa wa Takukuru walikamata bahasha ambazo juu zilikuwa zimeandikwa majina ya Wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT wa uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika kesho mjini hapa.
Viongozi wanaoadaiwa kukamatwa pamoja na mkuu huyo wa wilaya ni Katibu wa UWT mkoani Kilimanjaro, Mariam Sagita, Katibu wa UWT wilaya ya Moshi mjini, Hadija Ramadhani na Hawa Sultani ambae ni mfanyabiashara.
Kwa mujibu wa Budigila, wajumbe ambao ni wapiga kura za maoni ya Ubunge viti maalumu walikuwa wakiingia kwa zamu katika chumba hicho ambapo walikuwa wakipewa kati ya sh50,000 na 100,000 kulingana na uzito wa mjumbe.
Hata hivyo akizungumza na waandishi wa habari baadae jana mchana katika Hosteli ya Umoja inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), Machangu alikanusha tuhuma zote zilizoelezwa na Takukuru.
Machangu alifafanua kuwa siku hiyo akiwa njiani kuelekea katika hoteli hiyo saa 10:00 jioni, alikutana na watendaji hao wawili wa UWT mkoa na wilaya ambao waliona ni vyema wakapate chakula cha mchana pamoja.
“tulifika pale saa 10:00 na sio saa 8:00 kama Takukuru wanavyodai na tulipofika pale tukakuta eneo lote la hoteli liko full booked (limejaa) kwa hiyo kwa sababu za kiusalama nikaona nikodishe chumba kimoja tukitumie”alisema.
Dk.Machangu alisema sababu za kumfanya achukue tahadhari za kiusalama ni kutokana na tukio lililomtokea mwaka 2007 ambako alivamiwa na kunusurika kuuawa hivyo mahali popote anapokwenda anachukua tahadhari.
Alisema wakati chakula kilipokuja na kabla hawajaanza kula, ghafla mlango wa chumba walichokuwemo ulianza kugongwa katika hali ambayo haikuwa ya kistaarabu hali ambayo ilimfanya ahofie kufungua mlango huo.
“hakukuwa na suala lolote la rushwa kama Takukuru wanavyojaribu kuuleza umma…tatizo nimejengewa maadui wengi katika kinyang’anyiro hiki cha viti maalumu baada ya kuonekana nyota yangu inang’ara” alisema.
Alisema kutokana na nyota yake kung’ara, baadhi ya wagombea wanafanya mbinu za kummaliza kisiasa ili asiweze kushinda lakini akasema Mungu ndiye anayegawa riziki na anaamini wapiga kura wanaelewa kinachoendelea.
Alikanusha madai ya Takukuru kuwa amekuwa akitumia gari la ukuu wa wilaya ya Kasulu katika kampeni hizo na kusema gari hilo alilielegesha ofisi ya mkuu wa mkoa Kilimanjaro tangu Julai 12 aliporejea kutoka Dodoma.
Dk.Machangu aliitaka Takukuru kufanya uchunguzi wa kina katika suala hilo na kujiridhisha kabla ya kuamua kulipeleka suala hilo kwenye vyombo vya habari akisisitiza kuwa wakati wote amekuwa akisimamia maadili kikamilifu.
Comments