Sunday, July 04, 2010

Anayedaiwa kufa aibuka siku 40 baada ya kuzikwa




MAKAZI wa Msamvu mkoani Morogoro Khamisi Abdul  (47), aliyedaiwa kufariki Juni 9 mwaka huu na kuzikwa katika Makaburi ya Kola mjini humo, ameibuka huku akiwa hai.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bahati Abdul (24) ambaye ni mtoto wa Abdul alisema baba yake alifariki baada ya kujichoma na kisu tumboni na kwamba kabla ya mauti kumfika alipelekwa hospitalini na kulazwa.
 
"Baba alikuwa akijishughulisha na biashara  ya  kutembeza  sabuni mtaani  na alifariki Juni 9 baada ya kujichoma na kisu tumboni Mei 29 na ukweli hakuwa mgonjwa  wa  akili," alisema Bahati.
 

Akizungumza na waandishi wa habari jana Abdul ambaye alikuwa amepoteza  kumbukumbu  alisema anachokumbuka   ni kwamba alikuwa akilala  katika  pango lenye  nyoka na wanyama  wengi ambao hawakuweza kumdhuru.

 “ Mara nyingine nilikuwa natembea porini na kukutana na wanyama wakali, lakini cha kushangaza, wao ndio walikuwa wakinikimbia,” alisema Abdul
 
Alipoulizwa kuhusu familia  yake alisema anakumbuka alikuwa na watoto watatu kati  yao mmoja ndio wa kumzaa mwenyewe, wengine  wawili walikuwa watoto  wa  marehemu mkewe .
 
“Mtoto  wangu wa kumza anaitwa Muka Khamis,"  alisema Abdul kwa  shida .

Baadhi  ya  wafanyabiashara  katika soko la Sabasaba  ambako  Abdul  alikuwa akifanya biashara  walisema mara baada ta taarifa ya kifo cha Khamisi walitoa michango yao ya fedha.

Jalala  Uwezo  alisema alisema Khamisi alikufa mwezi Juni na walimzika katika makaburi ya Kola.
 
Tukio hilo lilivuta hisia za wengi mkoani humo, Nabii Joshua Aram wa  Kanisa  la Uponaji alimchukua  mtu  huyo na kwenda naye  maeneo ambayo anadaiwa  alikuwa akifanya biashara zake  kabla   ya kifo chake  ili kuthibitisha hali hiyo.

Akiwa huko kundi  la watu  walimzunguka  na kumshangaa  huku wengine  wakitokwa  na  machozi na kudai  kuwa alishakufa  na kwamba tangu alipofariki bado hazijatimia siku 40.
 
Akizungumzia  kupatikana kwa  Abdul, Nabii  Joshua   alisema wakiwa katika maombi  yao ya kawaida kuombea  wagonjwa nje  ya  uwanja  katika  eneo  la  Kihonda  Viwandani,   Abdul alitokea  akiwa katika  hali  kama   ya mgonjwa wa kichaa, akiwa na  nywele  na  ndevu  nyingi ambapo aliingia katikati  ya  uwanja  huku akipiga kelele.
 
Alisema   baadhi  ya waumini walidhani alikuwa  ni mtu mwenye matatizo  ya  akili,  lakini  waliendelea na  maombi  yao, ndipo mtu huyo alifika  katika eneo la mbele   la  maombi na kuanguka  chini .
 
“ Baada  ya  kuona  hali  hiyo  tuliendelea na maombi  mpaka hapo alipozinduka  na  kuanza kujishangaa  yeye mwenyewe. Wakati  huo hakuweza kuongea, hivyo  kuwafanya wanamaombi kuendelea  kumuombea",  alisema  Nabii  Joshua .
 
Alisema siku ya pili ya maombi  Abdul akiwa katika  uangalizi  wa kanisa  aliweza kujitambulisha, ndipo walipoamua kumpeleka nyumbani kwake na kubaini kuwa amefufuka. Imeandikwa na Lilian Lucas, Morogoro SOURCE: MWANANCHI

No comments: