Thursday, July 29, 2010

Kikwete awaapisha Naibu Makatibu Wakuu 9



RAIS Jakaya Kikwete jana amewaapisha Naibu Makatibu wakuu tisa katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Walioapishwa katika halfa hiyo ni Hussein Katanga, Maria Bilia, Nuru Milao, Balozi Herbert Mrango, Balozi Rajab Gamaha, Dk Yohana Budeba, Mbogo Futakamba, Ngosi Mwihawa na Job Masima.
Uteuzi wa maofisa hao waandamizi wa serikali ulifanyika julai 15, 2010 na rais Kikwete na kutangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo julai 20 mwaka huu.
Kwa mujibu wa uteuzi huo Katanga anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bilia anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Milao anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Balozi Mrango anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Balozi Gamaha anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Dk Budeba anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Futakamba anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mwihava anakuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais na Masima anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Wakizungumza na Mwananchi mara baada ya kuapishwa, Dk Budeba alimshukuru rais Kikwete kwa kumteua na kusisitiza kuwa kilichokuwa mbele yake ni kuhakikisha kuwa anatekeleza majukumu yote ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Imeandikwa na
Fidelis Butahe. SOURCE: MWANANCHI

No comments: