Mizengwe Yanga Kifukwe ajitoa dakika za mwisho



Mgombea Uenyekiti wa timu ya Yanga Francis Kifukwe ametangaza kujitoa kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Yanga huku akisema," Mimi ni mtuhumiwa wa basi la Yanga nimeifanyia mengi Yanga, lakini mnyonge mnyongeni haki yake mpeni kampeni nilidhani zimeisha tokea jana (juzi), lakini zinaendelea mpaka leo (jana)."

Baada ya kutangaza kujitoa vurugu zilitokea kwenye kambi ya Kifukwe ambapo watu wa kambi yake walianza kumtukana Ridhiwan na kulaani kauli aliyoitoa kwamba wanachama wasifanye makosa na kuchagua watu wanaokutana BAKURUTU.

Hata hivyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera aliingilia kati na kusema bado kamati haitambui mapinduzi ya Kifukwe kujitoa hivyo wale walio kambi ya Kifukwe watulie na uchaguzi uendelee na wanaomtaka Kifukwe wampigie kura na kama atashinda atatangazwa kuwa Mwenyekiti.

Bendera alifoka kwamba, "kuna njama zimepangwa na kikundi cha wanachama haiwezekani mtu ajitoe wengine mshikwe jazba, Kifukwe kajitoa muda ambao siyo muafaka, humu ndani Kifukwe hakuna kutoka mpaka kieleweke anayetaka kukupigia kura akupigie."

Baada ya Kifukwe kutangaza kujitoa mwanachama mmoja wa Yanga anayefahamika kwa jina la Hussein Makabureta aliangua kilio, huku wanachama wa kambi ya Kifukwe wengine waliondoka ukumbini bila kupiga kura na wengine walikuwa wakihamasishana kumpa Mbaraka Igangula kura zao.

Muda mfupi kupita Manji aliingia ndani akiwa na Kifukwe wanachama wanaompenda Kifukwe walimpigia makofi, lakini mfadhili huyo cha ajabu alitoka nje na wagombea wote wa nafasi ya mwenyekiti pamoja na Kifukwe halafu Manji akarudi tena akiwa na mabaunsa sita kwenda kupiga kura.

Inadaiwa kikao alichokifanya Manji na waliokuwa wakiwania nafasi ya mwenyekiti wa Yanga kilikuwa ni kuwashinikiza atakayechaguliwa kuwa mwenyekiti lazima amteue Kifukwe kuwa mjumbe wa baraza la wadhamini Yanga na Francis Kifukwe akichaguliwa kwenye nafasi hiyo lazima akubali ili kunusuru mpasuko ndani ya Yanga atakayekiuka Manji atajiondoa kuidhamini klabu hiyo. Taarifa zaidi baadaye

Comments