Monday, July 12, 2010

Mabasi ya mikoani
yaadimika Ubungo


ABIRIA wanaosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya bara wanalazimika kulipia nauli ya juu na wengine kukosa kabisa usafiri baada ya kutokea uhaba mkubwa wa mabasi kwenye Kituo Cha Mabasi cha Ubungo (UBT).
Kutokana na tatizo hilo magari madogo ya abiria maarufu kama daladala yamekuwa yakitumika kuwasafirisha baadhi ya abiria hao kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani.
Habari zimeeleza kuwa tatizo hilo la kwanza kubwa kutokea limesababishwa na mabasi mengi makubwa kukodishwa na wamiliki wa shule mbalimbali za sekondari kwa ajili ya wanafunzi wao wanaotarajia kuanza masomo leo.
Gazeti hili ambalo jana lilikuwa kituoni hapo kwa takriban saa sita lilikuta abiria wengi wakirudi nyumbani kutokana na kukosa usafiri, huku baadhi wakionekana kukata tamaa kabisa.
Mkuu wa kikosi cha polisi wa usalama barabarani kituoni hapo, Hassan Hassan alisema usafiri kituoni hapo umekuwa wa taabu tangu Ijumaa iliyopita.
“Nimefanya kazi hapa kwa kipindi cha miaka minne, lakini sijawahi kuona idadi kubwa ya abiria kama niliyoiona safari hii wakishindwa kusafiri. Watu ni wengi ajabu; sijui ni kutokana na maonyesho ya Sabasaba au mabasi kukodiwa na wanafunzi lakini ukweli abiria ni wengi waliokwama,” alisema Hassan.
Abiria hao walilalamika kuwa upungufu wa mabasi umesababisha kupanda kwa nauli na kusababisha abiria kuitupia lawama Sumatra na Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuchukua hatua kudhibiti ongezeko hilo la nauli.
“Tunakuja hapa tunaambiwa gari hakuna zipo coaster ambazo nauli yake ni Sh 30,000 hadi Sh35,000 gharama hizi ni kubwa na sisi tunashindwa kuzimudu,” alisema mama mmoja aliyekuwa akisubiri usafiri wa kwenda Arusha.
Hata hivyo mkuu huyo wa usalama barabarani kituoni hapo alisema tayari amekamata baadhi ya daladala hizo kwa kuwa hazina kibali cha kusafirisha abiria kwenda mikoani.
Alisema abiria wamekuwa wakirubuniwa na kukubali kutoa nauli kubwa lakini kwenye tiketi wanaandikiwa fedha kidogo, jambo linalotufanya askari kukosa ushahidi kwani kwenye risiti anaandikiwa Sh17,500 lakini anatoa Sh30,000 sasa utamsaidiaje huyu,” alisema Hassan.
Hassan alisema tatizo ni abiria kukubali kutoa fedha nyingi za nauli tofauti na nauli elekezi kutoka Sumtara.
Lakini mkuu huyo akasema kuwa upungufu wa ghafla wa mabasi umetokana na idadi ya abiria kuongezeka.
Alisema kutokana na sababu hiyo wakati mwingine ofisi yake imekuwa ikichelewa kuruhusu mabasi kutoka kituoni hapo kwa muda wa roba saa ili kusubili abiria ambao huchelewa kuingia kituoni humo kutokana na msongamano watu na magari.
Naye meneja mahusino kwa Umma wa Sumatra, David Mziray alisema ofisi yake haina taarifa juu ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia kuanzia leo. Imeandikwa na Geofrey Nyang’oro na Hussein Issa: SOURCE:MWANANCHI.

No comments: