Askofu Desmond Tutu kustaafu shughuli za umma



Askofu mkuu wa kanisa la Kianglikana Desmond Tutu ametangaza kustaafu kwake kutoka shughuli za umma.

Mshindi huyo wa tuzo ya Nobel alikuwa mtetezi mkuu wa haki za binadamu na alipinga utawala wa ubaguzi wa rangi Aparthied nchini Afrika Kusini .

Desmond Tutu ametaja kilele cha kazi yake, kuwa siku aliyomtangaza Nelson Mandela kama rais wa kwanza wa Afrika Kusini aliyechaguliwa kidemokrasia, mwaka wa tisini na nne.

Aliwaambia wanahabari kuwa ananuia kupumzika na familia yake akitimia miaka sabini na tisa mwezi Oktoba mwaka huu.

Miaka michache kabla Nelson Mandela aachiwe huru, wakati harakati za ukombozi kutoka utawala wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini zili shika kasi, Askofu Desmond Tutu alikuwa mstari wa mbele.

Wakati wa maandamano ya kupinga serikali hiyo dhalimu, alijitokeza na vazi lake rasmi akiongoza waandamanaji. Mara kadhaa vurugu zilizuka na aliweka maisha yake hatarini akijaribu kutuliza pande zote mbili, hapo ikiwa ni vikosi vya usalama na wandamanaji waliokuwa na jazba mno. Na sio wakati wote alifaulu au hata kusikizwa.

Mara kadhaa askofu huyo kwa kanisa la Kianglikana aliikemea serikali na kuikumbusha kuwa sera zake zilikuwa zinakiuka upendo wa Mungu ndio maana akapewa jina la askofu wa wanasiasa. Ni juhudi hizo ambazo zilichangia yeye kupewa tuzo ya amani ya Nobel mwaka wa 84. Na kwa heshima hiyo Rais Nelson Mandela alimpa jukumu la kuongoza Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini mwaka wa 95.

Comments

Anonymous said…
Bila shaka na Babu Museveni wa Uganda atafuata mfano huu, na pia Mugambe ambaye yumo bakuri moja na Museveni. Pia Mzee misshtuko upeleke Ujumbe huu kwa Museveni kabla ya uchaguzi!!!!!!!!!