Monday, April 26, 2010

MUUNGANO: Mkapa, Mwinyi wang'ara







UWANJA wa Uhuru leo ulifurika maelfu ya watu walioenda kushuhudia sherehe za maadhimisho ya Miaka 46 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hisia za umati huo zilionekana wakati marais wastaafu, Ali Hassani Mwinyi na Benjamini Mkapa walipoingia.
Umati huo ulilipuka shangwe za kelele na vifijo wakati viongozi hao walipoingia kwenye uwanja huo mkongwe kwa nyakati tofauti kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuingia na kuzunguka uwanja mzima akipunga mkono.
Mkapa, ambaye aliongoza serikali ya awamu ya tatu ambayo ilijipatia sifa ya kuinua uchumi na kuboresha miundombinu, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuingia uwanjani katika siku hiyo iliyokuwa na jua la vipindi.
Baada ya Mkapa, ambaye aliongoza nchi kwa sera aliyoiita ya "ukweli na uwazi", kuingia uwanjani hapo kwa gari la kifahari aina ya Range Rover (Vogue), kelela za shangwe na vigelegele zililipuka kutoka kwenye umati wa watu.
Mkapa aliyeingia uwanjani hapo majira ya saa 3:15 alipishana kwa takriban dakika 15 na kiongozi wa serikali ya awamu ya pili, Mwinyi ambaye pia aliamsha kelele za shangwe kutoka kwa watu waliohudhuria.
Kama ilivyokuwa kwa Mkapa, Mwinyi ambaye aliingia uwanjani hapo na gari aina ya Toyota Landcruiser (VX) alishangiliwa kwa nguvu tofauti na ilivyokuwa kwa viongozi wa serikali ya sasa, akiwemo Rais Kikwete.
Shangwe kwa viongozi hao zilirindima kutoka jukwaa la kijani ambalo lilikuwa limepambwa na watu waliokuwa wamevalia fulana na kofia zenye rangi ya bendera ya taifa la Tanzania.
Mkapa amekuwa hajitokezi hadharani mara kwa mara na wakati mwingine amekuwa akikosekana kwenye sherehe kubwa kama maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika.
Kutoonekana kwake hadharani kumekuwa kukitafsiriwa kuwa kunatokana na kuandamwa na tuhuma za ufisadi kwenye serikali yake, zikiwemo tuhuma dhidi yake za kufanya biashara akiwa Ikulu.
Mkapa, ambaye alifanikiwa kukusanya kodi na kulipa madeni yaliyosababisha wahisani kuisamehe nchi, amekuwa hajibu tuhuma hizo na mara ya mwisho alisema: "Siwezi kuzuia masikio yenu kusikia, lakini naweza kuuzuia mdomo wangu kusema."
Mwinyi, ambaye pia aliwahi kuwa rais wa Zanzibar, aliongoza nchi enzi za mageuzi ya kiuchumi na kisiasa na kujipatia jina la Mzee wa Ruksa.
Imeandikwa na Sadick Mtulya na Patricia Kimelemeta. SOURCE: MWANANCHI


&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&

Malaria yamgeuka Afande Sele





UGONJWA wa malaria umemgeukia mwanaharakati wa kupinga ugonjwa huo kupitia muziki nchini, Afande Sele hadi kulazwa katika hospitali binafsi ya Mashuda iliyopo maeneo ya Mwananyamala A, wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Afande Sele ambaye ni mfalme wa rhymes nchini alihjikuta akikumbwa na ugonjwa huo licha ya kujiandaa vyema kufanya onyesho la mfano la kupinga ugonjwa huo katika tamasha lililofanyika katika vfiwanja vya mmnazi mmoja jijini hapo.
Akizungumza na Mwananchi akiwa amelazwa katika hospitali hiyo huku akiwa ametundikiwa dripu la tatu la kwinini, Afande Sele alisema ugonjwa huo ulimuanza bila kujijua mara tu baada ya kufika jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita majira ya usiku ambapo alihisi kuumwa na tumbo.
“Nilikuwa nimeshafika Dar baadaye kidogo nikajisikia tumbo linauma na muda ulivyozidi kwenda lilizidi kuuma nikaamua kwenda kupima ndipo nikakutwa na malaria iliyoanzia tumboni ndipo nilipoanza matibabu baada ya kulazwa katika zahanati hiyo,’’ alisema Afande Sele.
Afande alisema hadi asubuhi ya saa mbili ya siku ya maadhimisho ya tamasha la malaria alikuwa amekwisha maliza dripu tatu za dawa hiyo, ambapo alilazimika kuomba ruhusa na kwenda kufanya onyesho huku akiumwa marelia.
“Unajua umuhimu wa tamasha la lo imenilazimu kuomba ruhusa kwa dakika kadhaa nikaenda kupafomu na kisha nikarudi kumalizia dripu la tatu ambalo ndilo la mwisho alisema afande,’’ alisema Afand Sele
Hata hivyo tamasha hilo lilifana kwa kupambwa na wasanii mbalimbali akiwemo Afande Sele, Profesa Jay, Banana Zoro na wasanii kutoka THT.
Naye Waziri wa Afya, Profesa Mwakyusa alisema watu wengi wanaugua malaria kwa kuwa hawajingi na mbu waendezao ugonjwa huo na wengine hawachukui hatua za kuwakinga watoto wadogo ili wasipatwe na ugonjwa huo. Hata hivyo waziri huyo alisema Serikali inampango wa miaka mitano wa kuondoa ugonjwa huo hadi ifikapo mwaka 2015 ambapo zaidia ya 50 inatarajiwa kufikiwa. Imeandikwa na Festo Polea; SOURCE: MWANANCHI

No comments: