Monday, April 05, 2010

Breaking Newwssss:: Mwandishi mkongwe Konga afariki Dunia

MWANDISHI wa habari mkongwe na mchambuzi wa masuala ya siasa, jamii na utawala, Aristariko Konga amefariki dunia.

Taarifa zilizopatikana jana hospitalini Lugalo alikokuwa amelazwa takribani wiki mbili zilizopita zilieleza kuwa Konga alifariki dunia jana majira ya saa kumi jioni baada ya hali yake ya kiafya kubadilika ghafla.

Akizungumza na Mwananchi, Shemeji ya marehemu Konga, Godlove Ndingala alisema kuwa shemeji yake alifariki dunia jana jioni baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda.

"Ndugu yangu ni kweli yametufika, shemeji Konga ameaga dunia majira ya saa kumi hivi, hapa unapozungumza na mimi ni dakika chache tumetoka kupata uthibitisho wa kitabibu kuhusiana na kifo hicho,"alisema.

Alisema mipango zaidi ya mazishi ya marehemu Konga inafanyika, lakini kwa sasa msiba utakuwapo nyumbani kwa marehemu eneo la Ubungo Kibo karibu na baa ijulikanayo kama Kipembele.

"Kikao cha familia bado hakijakaa, lakini kwa kuanzia ni kwamba msiba utakuwapo nyumbani kwake kule Ubungo Kibo,"alisema Ndingala.

Historia ya Konga si nyepesi kuielezea, lakini amepata kuwa mwandishi na Mhariri Mwandamizi wa kampuni zinazochapisha magazeti ya Mwanahalisi, Mwananchi, Raia Mwema na The Guardian.

Konga atakumbukwa kwa ujasiri wake katika kusimamia mambo ya msingi kwani wakati fulani aliunguliwa nyumba katika mazingira ya kutatanisha suala ambalo lilidhaniwa kuwa uunguaji huo ulikuwa ni shambulio la kulipiza kisasi dhidi ya msimamo wa gazeti hilo katika masuala kadhaa ya kitaifa.

Nyumba iliungua na kuteketeza mali zote isipokuwa godoro na kitanda vilivyokuwa katika chumba cha watoto kilichonusurika, na zaidi Konga alibakiwa na suruali mbili na shati moja zilizokuwa zimeanikwa katika kamba nje ya nyumba baada ya kufuliwa.Konga ameacha mke na watoto kadhaa. Kwa hakika medani ya habari imepata pigo. SOURCE: MWANANCHI

No comments: