Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mhe. Judith Suminwa Tuluka, amesema nchi yake imepata fursa ya kujifunza uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, ambao utakuwa chachu ya kuendeleza mipango ya ujenzi wa mji wa Serikali katika mji mkuu wa Kinshasa.
Mhe. Judith ameyasema hayo leo Novemba 4, 2026, jijini Dodoma, mara baada ya kutembelea Mji wa Serikali Mtumba na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika eneo hilo.
Ameshukuru ushirikiano unaoendelea kuimarishwa kati ya Tanzania na DRC, akieleza kuwa kupitia ushirikiano huo wamepata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yatakayosaidia katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi yao.
Aidha, ameupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini DRC kwa kuendelea kuwa karibu na nchi hiyo, akibainisha kuwa hata baada ya kuteuliwa kushika nafasi ya Waziri Mkuu, ubalozi huo ulikuwa miongoni mwa taasisi za kwanza kumpongeza.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Anjela Kairuki, amesema Tanzania imefurahishwa na ziara hiyo, akieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni wa muda mrefu na nchi hizo zimekuwa na udugu unaozipa nafasi ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali.
Amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na DRC katika masuala mbalimbali ya maendeleo kulingana na uwezo na fursa zilizopo.
Waziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka ameambatana na ujumbe wake, ukiwemo wa Waziri wa Ujenzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Bwana John Banza Lunda.
Ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na DRC, hususan katika kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mipango ya ujenzi wa miundombinu ya Serikali.

.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment