Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiagana na Viongozi mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kabla ya kuondoka nchini leo, tarehe 22 Novemba, 2026, kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa Ziara ya Kikazi ya siku mbili.
Akiwa Addis, Dkt. Samia atashiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, tarehe 23 Novemba, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunuku kamisheni kwa Maafisa wapya wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika hafla iliyofanyika Novemba 21, 2026, katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, mkoani Arusha.
Maafisa waliotunukiwa kamisheni ni wahitimu wa Kundi la 07/23 la Shahada ya Sayansi ya Kijeshi pamoja na Kundi la 73/25 la Kozi ya Kawaida ya Kijeshi (Regular), baada ya kukamilisha mafunzo yao katika chuo hicho.
Hafla hiyo pia iliambatana na mahafali ya saba ya kijeshi kwa wahitimu wa Kundi la 07/23 la Shahada ya Sayansi ya Kijeshi.
Katika sherehe hizo, Rais Dkt. Samia alikagua gwaride la heshima la Maafisa wanafunzi lililofanyika katika Uwanja wa Gwaride wa J.J. Mkunda, ndani ya Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli.
Aidha, Rais Dkt. Samia alikabidhi tuzo kwa wahitimu saba waliofanya vizuri zaidi katika mafunzo yao, wakiwemo watatu kutoka Kundi la Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na wanne kutoka Kozi ya Kawaida ya Kijeshi.
Hafla hiyo imekuwa sehemu ya hatua muhimu katika kuhitimisha mafunzo ya Maafisa hao na kuanza kwa majukumu yao mapya ya kijeshi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.



No comments:
Post a Comment