Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ,amewaagiza wenye leseni za uchimbaji madini kuzifanyia kazi kwa mujibu wa masharti yake, akionya kuwa Serikali itachukua hatua iwapo masharti hayo hayatatekelezwa.
Makamu wa Rais ametoa onyo hilo, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kusimamia katazo la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi. Amezitaka kampuni za ndani na nje kuwekeza katika viwanda vitakavyochakata madini hapa nchini hadi hatua ya bidhaa za mwisho. Amesema uwekezaji huo utapanua fursa za ajira, utatoa malighafi kwa viwanda na kuongeza mapato ya Taifa.
Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya wadau 1,700 kutoka ndani na nje ya nchi kujadili namna ya kuongeza uchakataji wa madini nchini ili kukuza viwanda, kuongeza ajira na mapato ya Taifa.
Wizara ya Madini imeandaa mkutano huo kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania.Majadiliano yanahusu fursa za uwekezaji katika dhahabu, kinywe, nikeli, shaba, madini adimu na niobiamu, pamoja na namna ya kuongeza ushiriki wa wachimbaji wadogo na kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa madini.











No comments:
Post a Comment