Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 6, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Afrika Kusini nchini, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe, anayemaliza muda wake wa utumishi nchini, pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni ya Thirty-Five Investment Holding ya Doha, Qatar, Dkt. Khalid bin Mohammed bin Abdullah Al Attiyah, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo na Balozi Mayende-Malepe, Rais Samia amempongeza kwa kukamilisha muda wake wa utumishi nchini na kumshukuru kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Balozi Mayende-Malepe amemshukuru Rais Samia, Serikali na wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano na ukarimu alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake, akieleza kuwa Tanzania imekuwa na nafasi ya kipekee katika maisha yake kutokana na uhusiano wa kihistoria na kindugu kati ya mataifa hayo mawili.
Aidha, Balozi huyo amepongeza mchango wa Tanzania katika masuala ya kikanda na kimataifa na kuyakaribisha makampuni ya Tanzania kutumia fursa za biashara na uwekezaji nchini Afrika Kusini.
Rais Samia ameeleza kuwa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini imeongezeka katika kipindi cha utumishi wa Balozi huyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amefanya mazungumzo na Dkt. Khalid Al Attiyah kuhusu fursa za uwekezaji nchini Tanzania, hususan katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi na miundombinu ya usafiri.
Dkt. Al Attiyah ameeleza nia ya kampuni yake kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na ufugaji wa ng'ombe katika eneo la Kongwa mkoani Dodoma, pamoja na uvuvi wa bahari kuu, uchakataji na uhifadhi wa samaki katika Bandari ya Uvuvi Kilwa.
Vilevile, kampuni hiyo inatathmini fursa za uwekezaji katika miundombinu ya usafiri Zanzibar, ambapo majadiliano ya awali tayari yameanza kati ya wawakilishi wa kampuni na wataalamu wa taasisi husika.
Rais Samia amezitaka taasisi zinazohusika kuendeleza majadiliano hayo kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kubaini miradi inayoweza kutekelezwa kwa manufaa ya pande zote.
Mazungumzo hayo yameonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kimataifa, kupanua ushirikiano wa kibiashara na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi nchini.






No comments:
Post a Comment