Wahariri wa vyombo vya habari nchini, kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wamefanya ziara katika Hifadhi ya Ngorongoro na kujionea vivutio vya kipekee vinavyosimulia historia ya binadamu, maajabu ya asili na utajiri wa urithi wa Tanzania.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa TEF, Bw. Deodatus Balile, wahariri hao walitembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi hiyo, ikiwemo Bonde la Olduvai, ambako walipata maelezo kuhusu ushahidi wa kisayansi unaothibitisha uwepo wa binadamu wa kale, pamoja na kushuhudia simulizi ya ajabu ya mchanga unaohama, mojawapo ya vivutio vya kipekee vya Ngorongoro.
Akizungumza na wahariri hao, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Abdul-Razaq Badru, amesema Ngorongoro inaendelea kuwa kivutio muhimu cha utalii kutokana na utajiri wake wa maliasili, historia na urithi wa kiutamaduni unaoitofautisha na maeneo mengine duniani.
Amesema katika kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, mamlaka hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha Ngorongoro inakuwa miongoni mwa maeneo yatakayowavutia wageni watakaowasili nchini kwa ajili ya mashindano hayo.
Katika kufanikisha azma hiyo, Dkt. Badru ameeleza kuwa juhudi zinaelekezwa katika kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha mifumo ya malipo, kujenga barabara kutoka Geti la Loduare hadi Seneto, pamoja na kuboresha kivutio cha maporomoko ya maji ya Endoro ili kuongeza ubora wa huduma na uzoefu wa watalii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Bw. Deodatus Balile, amesema Hifadhi ya Ngorongoro ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia mapato ya utalii, huku ikichangia pia maendeleo na ustawi wa wananchi.
Balile amesisitiza kuwa Jukwaa la Wahariri Tanzania litaendelea kushirikiana na kutoa ushauri wenye tija katika juhudi za kuendeleza na kuitangaza hifadhi hiyo, ili kuhakikisha urithi wake wa kipekee unaendelea kuwa chanzo cha fahari na manufaa kwa Taifa.
Ngorongoro si mahali pa kutazama wanyamapori pekee, bali ni hazina ya historia ya binadamu, maajabu ya asili na urithi unaoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo ya kipekee ya utalii duniani.
NGORONGORO – MAAJABU YA ASILI, HISTORIA INAYOISHI!
#Ngorongoro #TEF #AFCON2027 #UtaliiTanzania #VisitTanzania #OlduvaiGorge #TanzaniaUnforgettable






No comments:
Post a Comment