Madereva 27 wamekamatwa na kuwekwa mahabusu kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani, kufuatia operesheni maalumu ya ukaguzi wa magari iliyofanywa na Jeshi la Polisi katika eneo la Vigwaza, Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Operesheni hiyo iliyofanyika nyakati za usiku ilihusisha ukaguzi wa magari 210 na kuongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Julius Mwakabonga, Mkuu wa Operesheni kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani, akishirikiana na Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Edson Mwakihaba, kwa lengo la kudhibiti ukiukwaji wa sheria za barabarani.
Ametoa rai kwa wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanakuwa na madereva wawili kwa kila safari ili kuwezesha kubadilishana majukumu na kupata muda wa kupumzika.
Aidha, amewataka Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa (RTO) kuimarisha ukaguzi wa mabasi na kudhibiti ubebaji wa abiria wanaozidi idadi inayoruhusiwa, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kupewa upendeleo, bila kujali nafasi au cheo chake.
Katika hatua nyingine, Mwakabonga amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria, hasa kuelekea mwisho wa mwaka ambapo safari huongezeka, huku akionya kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwafuatilia wanaokiuka taratibu, wakiwemo madereva wa magari ya kubeba mchanga.
Amewahimiza abiria kutoa taarifa wanapobaini uzembe wa madereva ili kusaidia kuzuia ajali na kulinda maisha ya watu.


No comments:
Post a Comment