Friday, November 06, 2026

POSTA TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MWAKA WA PMI, YAWASILISHA UZOEFU WAKE WA USIMAMIZI WA MIRADI









Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeendelea kuonesha mchango wake katika kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi kwa kushiriki Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Wataalamu wa Usimamizi wa Miradi Tanzania (PMI Tanzania Project Management Week & Annual Conference 2026), uliofanyika Novemba 5, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Cate Hotel, mkoani Morogoro.

Mkutano huo ulilenga kuwakutanisha wataalamu wa usimamizi wa miradi, viongozi wa taasisi mbalimbali na wadau wengine kwa ajili ya kubadilishana maarifa, uzoefu, ubunifu na kujadili namna bora ya kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi nchini.

Katika mkutano huo, Shirika la Posta Tanzania lilipata nafasi ya kushiriki katika mjadala wa jopo (Panel Discussion) uliokuwa na mada isemayo “Project Management Office in the Public Sector” (Ofisi ya Usimamizi wa Miradi katika Taasisi za Umma), ambapo Meneja wa Ofisi ya Miradi wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Seleman Daffy, alikuwa mzungumzaji (Speaker), huku Mjumbe wa Bodi na Makamu wa Rais wa Masuala ya Wanaojitolea wa Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Miradi Tanzania, Bi. Rahma Kova, akiwa msimamizi wa mjadala huo (Moderator).

Akizungumza mara baada ya kushiriki mjadala huo, Bw. Daffy amesema, majadiliano hayo yalikuwa na manufaa makubwa, kwani yalitoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuonesha umuhimu wa taasisi za umma na binafsi kuwa na ofisi maalumu za usimamizi wa miradi.

Amesema kupitia mjadala huo, imeonekana kuwa taasisi nyingine zinaweza kujifunza kutokana na uzoefu wa Shirika la Posta Tanzania katika kutekeleza mfumo huo wa usimamizi wa miradi.

Kwa upande wake, Bi. Rahma Kova, amesema Posta ilipewa nafasi hiyo kutokana na kutambuliwa kwake kama miongoni mwa taasisi chache zenye ofisi maalumu ya usimamizi wa miradi, hivyo uzoefu wake ulikuwa muhimu kushirikishwa na wataalamu wengine waliohudhuria mkutano huo.

Kupitia ushiriki huo, Shirika la Posta Tanzania limepata fursa ya kutangaza uzoefu wake katika usimamizi wa miradi na kushiriki katika mijadala ya kitaalamu inayolenga kuimarisha utendaji wa taasisi, matumizi bora ya rasilimali na utekelezaji wenye tija wa miradi kwa maendeleo ya Taifa.

No comments:

POSTA TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MWAKA WA PMI, YAWASILISHA UZOEFU WAKE WA USIMAMIZI WA MIRADI

Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeendelea kuonesha mchango wake katika kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi kwa kushiriki Mkutano...