Wednesday, November 04, 2026

NCHI ZA EAC ZATAKIWA KUJIPANGA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO











Na Mwandishi Wetu – Nairobi, Kenya

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kuimarisha ushirikiano na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño, zikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, uharibifu wa miundombinu na kuathirika kwa biashara na maisha ya kawaida ya wananchi.

Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Wataalamu wa Sekta Mbalimbali kuhusu Maandalizi na Mwitikio wa Kikanda dhidi ya Mvua Zinazotarajiwa za El Niño Kali, unaofanyika Nairobi, Kenya, kuanzia Novemba 4 hadi 6, 2026.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa wataalamu  umeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala.

Akifungua mkutano huo Mratibu wa Mradi wa Pamoja wa Sekta Mbalimbali wa Usalama wa Chakula na Lishe wa Uganda, Bw.Julius Twinamatsiko amesema utabiri unaonesha uwezekano wa mvua kunyesha kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026, hali inayohitaji maandalizi ya haraka na hatua za pamoja.

Amezitaka nchi wanachama kubaini maeneo hatarishi katika miundombinu ya usafirishaji, kuandaa njia mbadala, kuhakikisha upatikanaji wa chakula na malisho ya mifugo, pamoja na kuimarisha huduma za afya na ufuatiliaji wa magonjwa yanayoweza kuenea kutokana na mafuriko.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Sekretarieti ya EAC amesisitiza kuwa athari za El Niño zinaweza kuhatarisha amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi, hivyo juhudi za kila nchi zinapaswa kuunganishwa kupitia mpango wa pamoja wa kikanda.

Mkutano huo unalenga kutathmini uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na athari zinazotarajiwa, kubaini mapungufu na kuandaa mpango wa uratibu wa kikanda utakaosaidia kulinda maisha ya wananchi, huduma muhimu na shughuli za biashara katika Afrika Mashariki.

No comments:

DKT. MWIGULU AKUTANA NA WAZIRI MKUU WA DRC

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemkorasi ya Kongo (DRC), Judith Suminwa Tuluka na wamejadiliana n...