Thursday, November 19, 2026

RAIS SAMIA: TUSHINDANE NA DUNIA, SIYO SISI KWA SISI

 









Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuunganisha nguvu katika uzalishaji wa viwandani, badala ya kushindana zenyewe kwa zenyewe, ili kujenga uchumi imara na kuongeza ushindani wa bidhaa katika masoko ya kimataifa.

Rais Samia ametoa wito huo leo, Novemba 19, 2026, nchini Uganda, wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kiwanda cha Kuunganisha Magari cha Double Q Motor Assembly Plant, akiwa pamoja na mwenyeji wake, Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesisitiza kuwa wakati umefika kwa nchi za Afrika Mashariki kutumia rasilimali na uwezo wake wa uzalishaji kujenga viwanda vinavyosaidiana na kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda.

“Tunapaswa kushindana na dunia, sio sisi kwa sisi,” amesisitiza Rais Samia.

Amesema uwekezaji wa kiwanda hicho nchini Uganda ni hatua muhimu katika kukuza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa magari yaliyotumika yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.

Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa soko kubwa la Jumuiya ya Afrika Mashariki linatoa fursa muhimu kwa viwanda vya ukanda huo, huku akibainisha kuwa Bandari ya Dar es Salaam imeongeza uwezo wake wa kupokea takribani tani milioni 33 za shehena.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Tanzania inaendelea kutafuta ubia na wawekezaji kwa ajili ya kuanzisha uzalishaji wa injini za treni nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza viwanda na kuongeza thamani ya uzalishaji wa ndani.

Kwa upande wake, Rais Yoweri Museveni amepongeza uwekezaji wa kampuni za Double Q na Sinotruk nchini Uganda, akisema hatua hiyo inaongeza thamani ya uzalishaji wa ndani kwa asilimia 20.

Rais Museveni amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Uganda kutumia kwa pamoja rasilimali zinazokamilishana, hususan gesi inayopatikana Tanzania na madini ya chuma yaliyopo Uganda, ili kuimarisha viwanda na biashara.

“Tanzania ina gesi, Uganda ina madini ya chuma. Tukiziunganisha rasilimali hizi, tutafanya biashara bora na kufanikiwa kwa urahisi zaidi,” amesema Rais Museveni.

Viongozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi, soko la pamoja na kuimarisha uzalishaji wa kikanda kama msingi wa kuongeza ajira, kupanua biashara na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa Afrika Mashariki.

No comments:

RAIS SAMIA: TUSHINDANE NA DUNIA, SIYO SISI KWA SISI

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuunganisha n...