Wednesday, November 04, 2026

DKT. MWIGULU AKUTANA NA WAZIRI MKUU WA DRC








WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemkorasi ya Kongo (DRC), Judith Suminwa Tuluka na wamejadiliana njia mbalimbali za kuimarisha uchumi baina ya nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma leo (Jumatano, Novemba 04, 2026), Dkt, Mwigulu amesema Tanzania na DRC zina fursa ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi katika nyanja mbalimbali ikiwemo madini, usafirishaji na uchukuzi, chakula na utoaji wa huduma za afya.

“Bado kuna fursa kubwa ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa yetu mawili. Kama ujuavyo, Tanzania na DRC ni mataifa yaliyobarikiwa kuwa na utajiri mkubwa, ikiwemo madini, ardhi yenye rutuba, misitu, maziwa na mito.”

Akielezea uwepo wa fursa za kibiashara, Waziri Mkuu Mwigulu amesema nchi hizo bado zinaweza kuongeza kiwango cha sasa  cha biashara ikiwa watahamasisha sekta binafsi kutumia fursa zinazotolewa na mifumo ya kikanda na ya bara. “Tanzania na DRC tuna nafasi chanya nyingi za kufanya biashara zaidi. Tutawatuma mawaziri wa sekta zinazohusika ili waendelee kukutana na kukamilisha hayo masuala,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema DRC ni mtumiaji namba moja wa Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa na mchango wa asilimia 48 ya shehena yote ya mizigo ya nchi zisizo na bandari na akatumia  fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu wa DRC kwa kutenga muda na kutembelea bandari hiyo.

“Nimefurahi kwenye ziara hii umepata fursa ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu ya Kwala, ambako tumetoa eneo kubwa kwa DRC. Kipekee nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya DRC kwa uamuzi wake wa kujenga barabara kutoka Lubumbashi kuja Kalemie. Hatua hii itafungua fursa za kibiashara kwa upande wa Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa DRC, Judith Suminwa Tuluka aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa misaada yote iliyoipatia nchi hiyo ikiwemo ya kijeshi, kutunza wakimbizi na vyakula na vifaa tiba wakati nchi hiyo ilipopata maafa.

“Tunaishukuru na Serikali ya Tanzania na hasa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kupitia vikao mbalimbali vya kikanda na kimataifa alipambana na kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo iweze kubaki na amani,” alisema na kuongeza:

“Hatuwezi kuisahau Tanzania kwa kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi zaidi ya 90,000 wakati nchi yetu ilipokuwa inapambana na Rwanda. Tunaishukuru sana Tanznaia kwa mshikamano huo.”

Akielezea mafanikio ya nchi hiyo, alisema wamefanya mageuzi ya kiuchumi kupitia programu mbalimbali za ndani na nje. “Tumefanya mageuzi katika mfumo wetu wa kifedha na tukafanikiwa kujenga imani yetu kwenye medani za kimataifa. Faranga imepanda thamni ikilinganishwa na dola ya Marekani. Wakati naingia ofisini Juni 2024, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na Faranga 3,000 lakini hivi sasa dola moja ni sawa na Faranga 2,250.”

Alisema kutokana na hali hiyo, nchi yao imefanikiwa mikopo ya Dola za Marekani milioni moja na imeanza kujiondoa kwenye orodha ya nchi zenye madeni chechefu. “DRC kwa sasa ina imani chanya katika ngazi ya kimataifa,” alisisitiza

No comments:

DKT. MWIGULU AKUTANA NA WAZIRI MKUU WA DRC

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemkorasi ya Kongo (DRC), Judith Suminwa Tuluka na wamejadiliana n...