Mkurugenzi Mkuu Hamad Abdallah akitoa wasilisho kuhusu shughuli, mafanikio, maendeleo ya miradi na mikakati ya uwekezaji kwa wajumbe.
Viongozi kutoka Zanzibar wakisikiliza kwa makini wasilisho hilo.
Baadhi ya wakurugenzi wakifuatilia wasilisho la Mkurugenzi Mkuu.
Mkurugenzi wa Ujenzi Qs Dr. Godwin Maro (mbele mwenye koti jeusi) akifafanua jambo kwa wajumbe kuhusu mradi wa GPR.
Mkurugenzi Mkuu akiwaongoza wajumbe kujionea mradi wa Kawe 711.
Dar es Salaam, Novemba 20, 2026
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Mhe. Rahma Kassim Ali, Mhe. Rahma Kassim Ally, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, Ardhi na TEHAMA ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na uongozi wa Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), wamelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ubunifu, ubora na matumizi ya teknolojia za kisasa katika utekelezaji wa miradi ya nyumba ya Golden Premier Residence (GPR) na Kawe 711, iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Novemba 20, 2026, wakati wa ziara ya siku moja iliyolenga kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna NHC inavyotekeleza miradi ya makazi ya kisasa inayozingatia mahitaji ya wananchi, ubora wa ujenzi na mazingira rafiki ya kuishi.
Akizungumza baada ya kujionea miradi hiyo, Mhe. Rahma amesema NHC imeonesha mfano mzuri wa namna taasisi za umma zinavyoweza kutumia ubunifu na utaalamu katika kuendeleza miradi ya nyumba yenye viwango bora, huku ikichangia kubadilisha mandhari ya maeneo inayotekelezwa.
Ameeleza kuwa ziara hiyo imewapatia maarifa na uzoefu muhimu kuhusu upangaji wa miradi, usanifu wa majengo, matumizi bora ya maeneo na ujenzi wa makazi yanayokidhi mahitaji ya maisha ya sasa.
"Tumejifunza mengi kutoka NHC kuhusu namna ya kuendeleza miradi ya makazi bora, yenye ubunifu wa kisasa na miundombinu rafiki kwa wananchi," amesema Mhe. Rahma.
Akiuzungumzia mradi wa Kawe 711, Waziri huyo ameeleza kuvutiwa na namna mradi ulivyopangwa na kutekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya makazi, huku akibainisha kuwa maendeleo ya miradi hiyo yamechangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mwonekano wa eneo la Kawe.
ZHC: NHC IMEKUWA SHAMBA DARASA KWETU
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), Bw. Sultani Saidi Suleimani, amesema miradi ya NHC imekuwa shamba darasa muhimu kwa taasisi yao kutokana na namna ilivyobuniwa na kutekelezwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya makazi ya wananchi.
Ameeleza kuwa uzoefu walioupata utawasaidia katika kubadilishana maarifa na kuangalia namna ya kuboresha mipango na utekelezaji wa miradi ya nyumba Zanzibar.
Kauli hiyo inaonesha umuhimu wa taasisi za umma za Tanzania Bara na Zanzibar kushirikiana, kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kutumia uzoefu uliopo katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
GPR NA KAWE 711 ZAWAVUTIA WAJUMBE
Katika mradi wa Golden Premier Residence (GPR), ujumbe huo ulipata fursa ya kujionea maendeleo ya ujenzi na kupewa maelezo kuhusu usanifu wa majengo, viwango vya ubora na matumizi ya teknolojia za kisasa katika ujenzi wa nyumba za makazi.
Aidha, katika mradi wa Kawe 711, wajumbe walijionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa ujenzi na kupata ufafanuzi kuhusu namna mradi huo unavyochangia kuongeza upatikanaji wa makazi bora na kuboresha mandhari ya eneo la Kawe.
Miradi hiyo miwili ni sehemu ya juhudi za NHC za kuendeleza makazi ya kisasa, kuongeza thamani ya maeneo na kuchangia ukuaji wa sekta ya nyumba nchini.
NHC YAHAIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA ZHC
Akizungumza na ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amewashukuru Waziri, Wajumbe wa Kamati na uongozi wa ZHC kwa kufanya ziara hiyo na kuonesha nia ya kujifunza kutokana na uzoefu wa Shirika.
Amesema NHC itaendelea kuimarisha ushirikiano na ZHC katika kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu za kuendeleza miradi ya nyumba kwa manufaa ya wananchi.
Aidha, ameahidi kufanya ziara Zanzibar ili kujionea shughuli na miradi inayotekelezwa na ZHC, hatua itakayosaidia kuimarisha zaidi mahusiano na ushirikiano wa kitaasisi.
USHIRIKIANO WENYE MANUFAA KWA WANANCHI
Ziara hiyo imefungua fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya NHC na ZHC katika maeneo ya usanifu, ujenzi, uwekezaji, usimamizi wa miradi na mikakati ya kuongeza upatikanaji wa makazi bora.
Ushirikiano huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa unaziwezesha taasisi hizo kubadilishana uzoefu na kutumia mbinu zilizofanikiwa katika kuboresha huduma za makazi kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Ujumbe huo uliongozwa na Waziri wa Ardhi Zanzibar, Mhe. Rahma Kassim Ally, ukiwajumuisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, Ardhi na TEHAMA ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mihayo Juma Nhunga, wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na uongozi wa ZHC.







No comments:
Post a Comment