Tuesday, December 06, 2016

SERIKALI YAWATAKA WATENDAJI NA WAMILIKI WA MITANDAO YA KIJAMII BLOGGERS KUZINGATIA NSHERIA ZA NCHI

1

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO-Dar es Salaam
SERIKALI imetoa wito kwa  wamiliki na watendaji wa mitandao ya kijamii (Blogs) nchini kufuata Misingi, Sheria na Maadili ya taaluma ya habari.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Idara ya Habari(MAELEZO) Hassan Abbas wakati wa uzunduzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Tanzania Bloggers Nertwork(TBN) na mafunzo kwa wanachama hao kuhusu uendeshaji wa mitandao ya jamii kwa manufaa.
Mkurugenzi Abbas alisema kuwa Blogger ni mwandishi wa habari, mwanahabari, na mwanataaluma ya habari hivyo anawajibu wa kuhakikisha anaandika na kusambaza taarifa zenye ukweli kwa manufaa ya nchi.
“mitandao ya kijamii inalisha sehemu kubwa ya taarifa duniani hivyo wamiliki na watendaji wanapaswa kufuata misingi mikuu mitatu ya uandishi wa habari, ambayo ni ukweli, ukweli, ukweli ili kuweza kuheshimika na kusonga mbele” alifafanua Abbas.
Aidha  Abbas amewataka watendaji wa Blogs kushirikiana na Serikali  katika kutoa Elimu kwa umma kuhusu Sheria ya Huduma ya Habari iliyopitishwa hivi karibuni.
Akijibu baadhi ya changamoto zinazowakabili wamiliki wa mitandao ya kijamii, Abbas alisema, ametoa rai kwa vyombo vya habari pale watumiapo kazi zao wanapaswa kuwatambua au kuomba idhini kwa mmiliki wa picha au makala husika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa muda wa TBN Joachim Mushi alisema mkutano huo unalenga kuwafundisha wanachama juu ya uendeshaji mitandao ya kijamii kwa manufaa, upashaji habari kwa kutumia mitandao yao kwa kuzingatia maadili na namna ya kunufaika na mitandao hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Jamii Media Maxence Melo akiwakilisha mada kuhusu masuala mbalimbali ya umoja na mikakati ya kujenga chama alisema kuwa ili blogger kuweza kufika walipokusudia wanatakiwa kwenda na wakati.
Alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali za ndani na nje ya ya bidhaa ama kampuni kuweza kufa, hivyo wamiliki wa mitandao ya kijamii wanapaswa kuwa wabunifu na wafuatiliaji  ili kuweza kujua mteja anahitaji nini na kwa wakati gani.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Mitandao ya kijamii ni ajira, itumike kwa manufaa” ni matokeo mazuri ya ushirikiano kati ya TBN na wataalamu wa masuala ya habari na mitandao ya kijami.
Post a Comment