Saturday, December 10, 2016

MAKAMU WA RAIS AITAKA TAKUKURU KUONGEZA KASI KUBAINI WAHALIFU WA VITENDO VYA RUSHWA

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO,DAR ES SALAAM.
 
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameitaka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuongeza kasi ya kuwabaini na kuchukua hatua za kisheria bila kuwaonea aibu na uoga wahalifu wa vitendo vya rushwa nchini.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu na uzinduzi wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam, Makamu wa Rais alisema mapambano dhidi ya rushwa hayajaelekezwa upande wa watumishi wa Serikali pekee, bali pia kwa wafanyabiashara pamoja na asasi za kiraia.

Samia alisema Serikali itaendelea kutambua mchango wa taasisi za uwajibikaji na utawala Bora katika jitihada zao za kuimarisha misingi ya Utawala bora, uwazi, uadilifu na  uwajibikaji.

Taasisi hizo ni Ofisi ya Rais-(Utumishi na Utawala bora), Takukuru, Sekretarieti ya Maadili, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tume ya Haki za binadamu, Mamlaka ya Ununuzi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

Aidha, Makamu wa Rais alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika taasisi hizo ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora za ukaguzi zenye kuleta tija kwa wananchi na hivyo kuimarisha uwajibikaji na thamani ya fedha kwenye makusanyo na matumizi ya rasilimali za umma.

“Serikali imeendelea kuziwezesha kiutendaji taasisi hizi ili kuhakikisha zina uwezo wa kukuza na kusimamia viwango vya maadili kwa kutoa elimu, kufanya uchunguzi, kupokea na kuhakiki matamko ya mali na madeni ya viongozi wa umma kwa lengo la kutekeleza falsafa ya utawala bora” alisema Samia.

Akifafanua zaidi Makamu wa Rais alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa baadhi ya watumishi na watendaji wa Serikali wamekuwa  wakiwabambikia kesi wananchi wasio na hatia kwa kupata hukumu zisizostahili, kitendo kinachopelekea kukwamisha maendeleo ya taifa.

Aliongeza kuwa Serikali katika kuhakikisha inalinda rasilimali za umma, inaondoa uonevu na dhuluma, kwa kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ili kukabiliana na tatizo hilo.

“Ni jukumu na wajibu wetu kama Serikali kutoa Ulinzi, Usalama na Huduma Bora kwa jamii, lakini ufanisi wa kutekeleza wajibu huu utawezekana endapo watumishi wote wa Serikali watawajibika ipasavyo kuwaongoza katika utendaji kazi” aliongeza Mama Samia.

Kwa upande wake Mkurugezi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Valentino Mlowola alisema kuwa maadhimisho hayo yamelenga katika kuimarisha nidhamu kwa watumishi wa umma kwa kuzingatia kasi ya maendeleo ya Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga alisema kuwa ni mara ya kwanza kwa kampeni hii kufanyika nchini kwa lengo la kihimiza ukuzaji wa maadili katika utumishi wa umma na katika jamii kwa ujumla, utetezi na ulinzi wa haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa, wizi, ufusadi na ubadhilifu wa mali za umma.

Kampeni ya siku ya Maadili na Haki za binadamu yenye iliyobeba kauli mbiu “kujenga na kukuza Maadili, Haki za Binadamu, Uwajibikaji, Utawala Bora na Mapambano dhidi ya Rushwa” imedumu kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Novema 10 hadi 10 Desemba mwaka huu.

No comments: