Thursday, December 08, 2016

KOCHA WA ZAMANI WA YANGA AULA TIMU YA TAIFA YA TRINIDAD & TOBAGO.

tom-vs-cabna

Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amejiunga na timu ya taifa ya Trinidad na Tobago, Shirikisho la Soka la nchi hiyo limemtangaza mjini Port of Spain.

Saintfiet anayechukua Stephen Hart aliyefukuzwa,amesaini mkataba wa miaka miwili, wakati Carolina Morace wa Italia anachukua majukumu ya timu ya taifa ya wanawake.

Huku T&T kwa sasa ikishiriki hatua ya mwisho ya mchujo wa kufuzu Kombe la Dunia kwa CONCACAF na ikiwa haina hata pointi moja baada ya mechi mbili, ujio wa Saintfiet unaweza kuinua kiwango cha timu na kupata matokeo mazuri katika mechi mbili zijazo za ugenini na Panama Machi 24 na Mexico Machi 28.

Rais wa TTFA, David John Williams alisema: “Kama hatapata matokeo mazuri katika mechi mbili zijazo tutamfukuza kwa sababu tutakuwa tumetolewa kwenye mbio za kuwania tiketi ya Kombe la Dunia tusipopata matokeo mazuri,”.

Saintfiet, mwenye umri wa miaka 43, alichezea vigogo wa Ubelgiji enzi zake, FC Boom kuanzia mwaka 1983 hadi 1997 kabla ya kuwa kocha akiwa ana umri wa miaka 24, akiweka rekodi ya kocha kijana zaidi kuwahi kutokea katika soka ya Ubelgiji.

Pamoja na Yanga aliowaachia Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2012 baada ya miezi miwili ya kuwa kazini, pia amefundisha timu nyingine nyingi zikiwemo klabu na za taifa katika nchi za Ujerumani, Finland, Jordan, Qatar, Ubelgiji, Uholanzi, Zimbabwe, Ethiopia and Namibia, Togo na Bangladesh.

Kwa upande wake, Carolina Morace mwenye umri wa miaka 52 ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Italia ambaye pia amechezea klabu mbalimbali za wanawake Serie A na alikuwa mfungaji bora katika michuano ya nyumbani kwao msimu wa 1984-1985, kabla ya kuendeleza makali yake kuanzia msimu wa 1987-1988 hadi 1997-1998.

Baada ya kustaafu akaanza ukocha Lazio kabla ya kufundisha timu timu ya taifa ya wanawake ya I]talia kuanzia 2000 hadi 2005, na timu ya taifa ya wanawake ya Canada kuanzia mwaka 2009 hadi 2011.

No comments: