Watoto wafa kwenye disko mkesha wa Idd


WATOTO wawili wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa vibaya baada ya kukosa hewa ukumbini walikokuwa wamejazana kusherehekea sherehe za Idd.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa tukio hilo la pili kutokea wakati wa sherehe za Idd, lilitokea usiku wa kuamkia jana katika ukumbi wa disko wa Luxury Pub ulioko Temeke, jijini Dar es Salaam.

Oktoba mosi mwaka 2008, maafa ya aina hiyo yalitokea mkoani Tabora ambako watoto 19 walifariki dunia kwa kukosa hewa kwenye ukumbi wa Disco wa Bubbles unaomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) .

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, David Misime aliliambia gazeti hili jana kuwa tukio lililoua watoto wawili mkoani Dar es Salaam, lilitokea saa 2:30 usiku baada ya umeme kuzima.

"Baada ya umeme kuzimia watoto hao walianza kujazana kwenye mlango wa dharura ili watokea nje kufuatia geti kubwa kufungwa. Kimsingi walikufa kwa kukosa hewa na kukanyagana," alisema Kamanda Msime.

Kamanda Msime aliwataja watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Lilian Ellysangu (8) na Amina Ramadhani (7).

Kamanda Msime pia aliwataja watoto waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Salia Hemed (6) Issa Said (10) Bernad Joseph (6), Adina Adam (9), Rukia Hemed (14) na Hashimu Shamte(17) na kueleza kuwa wote wamelazwa katika hospitali ya Temeke.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, baadhi ya majeruhi hao wametibiwa na kuruhusiwa lakini, Omari Athumani (18), Latifah Balawa (13), Abdalah Muhaji (10), Lissah Mwamba (10), Abdalah Mlaji (10) na Mohamed Ally (14) wanaendeleana matibabu hospitalini hapo.

"Polisi inawashikilia watu kumi kufuatia tukio hilo na tayari tumeufunga ukumbi huo kwa muda usiojulikana huku tukiendelea na uchunguzi," alisema kamanda Msime.

Aliongeza: “Tunafanya uchunguzi tuone kama kuna uzembe ili tujue cha kufanya kwa kufuata sheria”.

Akisimulia kuhusu tukio hilo, Kamanda Msime alisema baada ya umeme kukatika watu walijazana katika mlangoni wa ukumbi hivyo kushindwa kutoka nje ya ukumbi kwa vile walikuwa wanatumia mlango mmoja ambao ni mdogo badala ya mkubwa.

Kamanda huyo alibainisha kuwa kisheria wamiliki wengi wa kumbi za starehe za watoto sheria wanatakiwa kufunge saa 12:00 jioni ili kuwapa fursa watoto hao kurudi nyumbani mapema.

"Tukio hili limetokea zaidi ya muda huu unaotakiwa kisheria. Hapa inaonyesha wenye kumbi za starehe wanajali pesa zaidi kuliko maisha ya watu na mali zao," alisema Kamanda huyo.

Baadhi ya watoto waliojeruhiwa katika tukio hilo waliliambia gazeti hili wakiwa hospitalini wanakoendelea na matibabu kuwa ndani ya umbi huo pia kulikuwa na watu wazima.

“Mara baada ya umeme kukatika tu watu walianza kurusha chupa za bia ambazo ziliwaumiza baadhi yao na kuwafanya wakimbilie mlangoni na kuanza kukanyagana,” alisema Rukia Hemed.

Alisema walipokuwa wanajaribu kutoka nje ya ukumbi huo, mlinzi aliwazuia mlangoni akieleza kuwa anahofia wezi kuingia ndani ya ukumbi.

Hashimu Shamte ambaye alivunjika mguu alisema umeme ulikuwa umezima ndani tu kwani walipotoka nje walikuta taa zikiendelea kuwaka
Alisema hali hiyo inamaanisha kuwa waliozima umeme ni watu waliokuwa wanahusika na ukumbi na wala sio kukatika kwa umeme wa Tanesco.

Mmoja wa marehemu Amina Ramadhani, alizikwa jana saa 7:00 mchana katika makaburi ya Mbagala jijini Dar es Salaam wakati mazishi ya Lilian Ellysangu yanasubiri mama yake mzazi ambaye yuko Arusha kwa matibabu.

Shangazi wa marehemu Lilian Ellysangu, Amina Athumani ndiye aliyetoa taarifa za mazishi hayo kufanyika baada ya mama mzazi wa marehemu.
Habari hii imeandaliwa na Hussein Issa, Pamela Chilongola na Hermenegildus Rwihula

Comments