Wednesday, September 08, 2010

Ujumbe wa Eid el-Fitr


Balozi Alfonso E. Lenhardt

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni muda ambao Waislamu duniani kote wanafunga, wanaswali na kufanya matendo mema. Aidha, ni wakati wa kutafakari na kuimarisha imani zao, kutenda mema, kuwasaidia wenye shida na kuwa na huruma. Kwa niaba ya Watu wa Marekani, ninapenda kuwatakia Waislamu wote wa Tanzania Eid el-Fitr njema. Muda huu wa kujitafakari unatukumbusha kuwa maadili ya Uislamu - wema, kujali wengine, kuhudumia jamii, ushirikiano na huruma ni amali ambazo sisi kama Wamarekani tunazithamini sana na ambazo kwa hakika zimechangia sana katika tamaduni nyingi duniani kote.
Kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Rodham Clinton hapo tarehe 7 September katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Wizara yake, historia ya Uislamu Marekani inaweza kupatikana nchini kote Marekani. Nchi yangu imejaaliwa kuwa na Waislamu waliozaliwa nchini Marekani pamoja na wale waliohamia kutoka duniani kote ikiwemo Tanzania. Dhamira yetu ya kulinda na kudumisha uvumilivu wa kidini ilianza toka mwanzoni kabisa mwa uanzishwaji wa taifa letu. Mabadiliko ya Kwanza ya Katiba ya Marekani yalipiga marufuku kuanzishwa kwa sheria yoyote inayokwaza uhuru wa mtu kufuata mafundisho ya dini yake na hivyo kuhakikisha kuwepo kwa uhuru wa kuabudu nchini kote. Kama alivyosema Rais Barack Obama wakati wa hafla ya Iftar iliyofanyika katika Ikulu ya Marekani hapo Agosti 13 mwaka huu, Balozi wa kwanza Muislamu nchini Marekani ambaye alikuwa akitoka Tunisia alialikwa na Rais Thomas Jefferson, ambaye aliandaa chakula cha jioni kwa wageni wake wakati wa magharibi kwa sababu kipindi hicho kilikuwa ni cha Ramadhani - na kufanya tukio hilo kuwa Iftar ya kwanza kuandaliwa na Ikulu ya Marekani - hiyo ilikuwa zaidi ya miaka 200 iliyopita. 
Katika ziara zangu kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi hii nzuri ya Tanzania nilipata heshima kubwa ya kutembelea Misikiti, kukutana na viongozi wa kidini na waumini wa Kiislamu ili kukuza urafiki na ushirikiano wetu. Niliguswa sana kuona utulivu na uzalendo wa hali ya juu miongoni mwa Watanzania wa imani zote.  Pengine jambo hili ni mojawapo kati ya mafanikio makubwa zaidi ya taifa hili, kama inavyoashiriwa na jina la moja ya miji yake mikuu - "bandari ya salama."   Wakati Ramadhani ikielekea ukingoni, tudumishe moyo huo wa kushirikiana na kusaidiana kama jamii moja ili watoto wetu, bila kujali wamezaliwa wapi na wanaabudu vipi waweze kupata fursa ya kuwa vile walivyopangiwa kuwa kwa jina la Mwenyeezi Mungu, na katika kuimarisha utu wetu.
Eid Mubarak.

Alfonso E. Lenhardt ni Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano waTanzania

1 comment:

emu-three said...

TWASHUKURU KWA UJUMBE HUU WENYE MANENO TIMILIFU.