Wednesday, September 22, 2010

Meja Jenerali Natepe afariki dunia


MMOJA wa viongozi 14 walioasisi na kutekeleza Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyoindoa serikali ya Kisultani visiwani Zanzibar Meja Jenerali Abdallah Said Natepe amefariki dunia jana mchana katika hospitali kuu ya jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, kifo hicho kimetokea jana mchana katika hospitali hiyo kuu ya jeshi la wananchi.

Taarifa hiyo ilimnukuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akieleza kushtushwa na kuhuzunishwa na kifo cha mwanamapinduzi huyo na alimtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuelezea jinsi alivyoguswa na kifo hicho cha Mzee Natepe.

“Kifo kimemchukua mwanamapinduzi, mzalendo na mwanachama wetu mwaminifu katika kipindi ambacho taifa na Chama bado kinamhitaji sana, kifo kimetunyang’anya tunu wakati huu tunaoelekea Uchaguzi Mkuu, ni huzuni kubwa kwetu, ni majonzi makubwa na hatuna neno kubwa linaloweza kuelezea huzuni hii,” Rais Kikwete alisema.

Rais alipokea taarifa za kifo cha Mzee Natepe leo mchana akiwa Njombe mkoani Iringa ambako yuko kwa ajili ya shughuli za kampeni.

Rais, kupitia kwa Katibu Mkuu wa CCM, pia alituma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu Natepe.

“Mzee Natepe amekua sehemu ya maisha yangu ya kisiasa, kijamii na amenipa malezi na maelekezo mengi nikiwa kama kijana wake na amekua moja ya nguzo yangu kubwa katika shughuli zangu za kisiasa na kikazi katika maeneo yote niliyotumikia nchi yangu," alisema Rais na kuelezea kwa masikitiko huzuni aliyonayo na kuwahakikishia kuwa yuko nao katika kipindi hiki kigumu.

“Tunamshukuru mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi ya kuishi na Mzee Natepe na kufanya naye kazi, tunamuomba Mungu amlaze Mzee wetu mahali pema peponi na kumpa pumziko la milele, Amina”.

1 comment:

zitto kiaratu said...

kama alitekeleza mapinduzi tunashukukuru lakini kuuwa wananchi wasio na hatia vipi, kama unaamini mungu lazima analipwa kwa ujasusi wake, kuhusu mapinduzi ya zanzibar wanannchi hatukuelezwa yaliyotokea asante kwa uzimifu wa habari wa mtakatifu nyerere, unaweza ukasoma historia yote kupitia africana website ya dr leon sullivan funded by microsoft!!!!