Wednesday, October 21, 2009

AG mpya aanza kazi kwa mkwara

Mwanasheria Mpya Jaji Frederick Mwita.
Seth Kamuhanda.



SIKU moja baada ya kuteuliwa na kisha kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mwanasheria Mkuu mpya wa Serikali, Jaji Frederick Mwita Werema alisema atahakikisha kuwa taifa haliingii mikataba mibovu.

Akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kuapishwa Ikulu jana, Werema alisema kwa msisitizo: "Rais aliyeniteua ndio anaujua msimamo wangu."

Werema aliyemrithi Johnson Mwanyika aliyestaafu kwa mujibu wa sheria, alisema kuwa atafanya kazi na kutekeleza wajibu wake mpya kulingana na kiapo alichokula mbele ya rais na Jamhiri ya Muungano wa Tanzania.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuapishwa, Mwanasheria Mkuu huyo alisema katika kutekeleza wajibu wake mpya hataki mashinikizo ya wanasiasa au mtu yoyote.

"Mashinikizo… Hayo yapo huwezi kufanya kazi bila hayo kuwepo; lakini aliyeniteua anajua msimamo wangu. ..Sitaki mashinikizo na sipendi kuhukumu bila ushahidi. Mnataka nirudie kiapo changu? Nawahakikishieni kuwa itafanya kazi kufuata kiapo changu," alisema Jaji Werema.

Alipoulizwa kuhusu kashfa ya kampuni ya Richmond (LLC) ambayo mtangulizi wake (Mwanyika) amehusishwa, Jaji Werema ambaye pia ni mtaalamu wa sheria za mikataba na biashara, alikata kulisemea hilo. Hata hivyo alisema hilo linafanyiwa kazi na wahusika.
Imeandikwa na Exuper Kachenje.

No comments: