Waliotimuliwa Chuo Kikuu warejeshwa
Na Tausi Mbowe wa Mwananchi
BAADHI ya wanafunzi waliofutiwa udahili na kufukuzwa masomo kutokana na kufanya vurugu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamerudishwa chuoni hapo baada ya uongozi wa chuo hicho kumuomba Waziri wa Elimu kubatilisha uamuzi wake wa awali.
Awali serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, mwishoni mwa wiki ilitangaza kuwafutia udahili wanafunzi 38 na kutangaza kuwa hawataruhusiwa kujiunga na chuo chochote nchini pia alitangaza kutimuliwa kwa wengine 300.
Uamuzi huo uliotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, katika kikao cha Bunge kilichokuwa kikiketi mjini Dodoma.
Wanafunzi 38 wa chuo hicho ambao walidaiwa kuongoza vurugu, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na shitaka ya kula njama na kusababisha fujo.
Taarifa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliyosainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Professa Rwekaza Mukandala ilisema kuwa uongozi wa chuo umefikia hatua hiyo kutokana na hali halisi inayoendelea chuoni hapo ambapo mpaka sasa kumeshindikana kupatikana kwa hali ya amani.
Professa Mkandala alisema kutokana na hali hiyo uongozi wa chuo umeamua kumuomba Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kubatilisha uamuzi wake wa awali na badala yake wanafunzi hao washughulikiwe kutokana na sheria za chuo kama zinazoonyesha.
Kwa mujibu wa Professa Mukandala, Waziri Maghembe amekubaliana na ombi la uongozi wa chuo hicho na kwamba wanafunzi hao watashughulikiwa kulingana na sheria za chuo na wale wasio na hatia wataruhusiwa kuendelea na masomo kama kawaida. kwa taarifa za kina soma Mwananchi la kesho.
Comments