Friday, April 04, 2008

Maiti iliyogombewa Dar yazikwa


Na Jackson Odoyo wa Mwananchi

HATIMAYE mwili wa marehemu Paul Goliama (40) umezikwa na ndugu zake ambao ni waumini wa dini ya Kikristo badala ya waumini wa Kiislamu katika makaburi ya Sinza, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi jana, Shemeji wa marehemu, Ibrahim Msumari, alisema mazishi ya marehemu Goliama yalifanyika jana majira ya saa 8:00 mchana katika makaburi ya Sinza, jijini Dar es Salaam kwa amani na utulivu.

Msumari alisema baada ya kutoka katika eneo la mazishi, watu wote walielekea nyumbani kwa marehemu walipoweka matanga ili kuungana na ndugu jamaa na marafiki wa familia ya marehemu.

Machi 28, ulizuka mzozo mkubwa wa kugombea maiti hiyo baina ya waumini wa dini hizo huku kila upande ukidai kuwa ndiye mwenye haki ya kuizika maiti hiyo.

Mzozo wa huo ulidumu kwa zaidi ya saa tano katika Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Jimbo la Kinondoni Usharika wa Sinza muda mfupi baada ya mwili wa marehemu kupelekwa kanisani hapo kuombewa sala za mwisho kabla ya mazishi.

Baada ya jitihata na busara za Mchungaji wa Kanisa hilo, Tuheri Tuheri pamoja na Imamu wa Msikiti wa Safwa za kujaribu kusuluhisha mzozo huo zilishindikana, Jeshi la Polisi iliamua kuuchukua mwili huo na kuurudisha katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam mpaka mahakama itakapotoa maamuzi kuhusu dini ambayo ilistahili kumzika marehemu.


Machi 31, ndugu wa marehemu waliamua kwenda kufungua kesi katika Mahaka ya Kinondoni kudai kuuzika mwili huo ambapo juzi mahakama ilitoa uamuzi kuwa mwili huo uzikwe na ndugu zake.

Sababu kubwa iliyosababisha ya mwili huo kugombewa na dini mbili ni kutokana na marehemu kubadili dini mwaka 2004 kutoka Ukristo kwenda Uislamu na hatimaye mwaka 2006 akabadili tena toka Uslamu kurudi Ukristo.

No comments: