Pichani baadhi ya wanafunzi walioshiriki mgomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana wakiwa mikononi mwa polisi, picha za mdau Salhim Shao
Na Pius Rugonzibwa wa Citizen
ASKARI polosi wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia (FFU) wametembeza mkong'oto kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliodaiwa kuchochea fujo na kuwahimiza wenzao kugomea masomo chuoni hapo.
Wanafunzi hao walipata kipigo hicho jana mchana na kusababisha baadhi yao kuumia na wengine kukamatwa kwa kusababisha fujo chuoni.
Kuitwa kwa askari hao kulitokana na wanafunzi hao kuendesha mgomo siku mbili kwa madai ya kutaka wenzao waliosimamishwa masomo warejee chuoni bila masharti.
Juhudi za uongozi wa chuo kuwataka wanafunzi hao warejee madarasani zalishindikana hiyo kuulazimu utawala kutoa taarifa Jeshi la Polisi kuomba msaada ndipo FFU walifika na kutembeza mkong'oto wa nguvu.
Kabla ya kipigo hicho kuanza, wanafunzi hao waliogoma walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali kushinikiza wenzao waachiwe ikiwa ni pamoja na wimbo wa taifa na kutoa hotuba za kuhamasisha
“Hatuwezi kuendelea na mosomo wakati wenzetu wako nje, huu utakuwa usaliti. Tukubaliane pamoja na tuungane kuwarudisha wenzetu vinginevyo hakieleweki hapa,” walisikika baadhi ya wanafunzi wakisema.
Rais wa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo (Daruso), Deo Daudi, alisema wanafunzi wengi hawataki kufuata utaratibu katika kudai haki zao, hivyo kusababisha hali hiyo.
Comments