Serikali itathmini safari za viongozi-Kigoda

bajetSERIKALI imetakiwa kufanya tathmini ya faida za safari zinazofanywa na viongozi mbalimbali nje ya nchi kutafuta wawekezaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, Dk. Abdallah Kigoda, alisema hayo alipochangia mada kwenye semina ya wabunge kuhusu mwongozo wa kutayarisha mipango na bajeti ya serikali kwa kipindi cha mwaka 2008/2009, iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Alisema kamwe Tanzania haiwezi kujikwamua kiuchumi kama haitakuwa na utaratibu wa kutathimini mipango yake pamoja na kuwashirikisha wananchi kumiliki uchumi wao.
Kigoda alisema ni vema ikafanyika tathimini ya wawekezaji waliokuja nchini tangu viongozi walipoanza kufanya safari za kuwasaka nje ya nchi.
Alisema bila kufanya hivyo taifa linaweza likajikuta linatumia fedha nyingi kuliko kile kinachopatikana katika ziara husika jambo ambalo ni hatari kwa ukuaji wa uchumi.
“Tuanze kufanya tathimini ya safari zinazofanywa za kuwatafuta wawekezaji, ili kujua wamekuja wangapi na kama hawajaja ni kwa sababu zipi,” alisema Kigoda.
Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir (CCM) alisema mipango mingi inayopanga na serikali imekuwa haitekelezeki na kila mwaka inapangwa mingine bila kuangalia mafanikio na hasara ya mipango iliyopita.
Alisema tatizo la wabunge kutokuhoji mafanikio na hasara ya mipango iliyopangwa miaka iliyopita imechangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa hali hiyo, hasa kwa watendaji wa serikali.
“Mipango hii inakuwa kama moto wa makuti unawaka kwa kasi kisha unaisha mara moja na sisi wabunge hatuhoji kwa nini mpango fulani umeshindwa,” alisema Mudhihir.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF), alisema ni aibu kwa Tanzania kuendelea kutegemea wahisani kusaidia bajeti, huku ina bandari tano ambazo hazitumiki ipasavyo.
Alisema kukosekana mipango thabiti na ufuatiliaji finyu ni miongoni mwa sababu zinazoifanya Tanzania kuendelea kuwa masikini siku hadi siku huku rasilimali za kuikwamua zipo.
Rashid alisema kufurika kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ni aibu kwa nchi kwani kuna uwezekano wa kuboresha bandari nyingine na zikatumika na nchi ikapata mapato zaidi.Habari hii na Salehe Mohamed

Comments