Saturday, March 27, 2010

Ajali ya Kibamba yaua familia moja


AJALI ya lori na basi dogo iliyotokea juzi Kibamba, Dar es Salaam iliua watu wawili wa familia moja akiwamo mjamzito na kusababisha mtoto mwingine kubaki yatima, imebainika.

Waliokufa ni mjamzito na mumewe ambaye alikuwa akimsindikiza mkewe siku hiyo kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhudhuria kliniki.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu wa kiume, Issa Ngoro, kaka yake kwa jina la Ibrahim Hussein Ngoro na mkewe Zainab Ali aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane ndio waliokumbwa na janga hilo.

Issa alisema kaka yake alikuwa mfanyakazi katika bandari ya Dar es Salaam na alikuwa na kawaida ya kudamka kuwahi kazini akichelea msongamano wa magari barabarani.

“Siku ya tukio, aliondoka alfajiri sana akifuatana na mkewe ili ampeleke kliniki Muhimbili kwanza ili kuwahi foleni ya wajawazito Muhimbili na barabarani na kisha naye awahi kazini kwake,” alisema Issa.

Alisema familia hiyo imeacha mtoto mmoja wa kike, Mwanaidi Ibrahim (4) na mimba aliyokuwa nayo ilikuwa ya uzao wa pili.

Aliongeza kuwa taarifa za ajali hiyo alizipata akiwa msikitini asubuhi, ambapo Imamu aliwatangazia kuwa kuna ajali eneo la darajani na kumlazimu kwenda kushuhudia ingawa hakuwa na uhakika kama alikuwamo ndugu yake.

“Nilipofika pale kwa kweli nilichanganyikiwa kwa jinsi maiti walivyokuwa wamekatikakatika na baada ya kuona mjamzito akitolewa, ndipo nikamwaza shemeji yangu, na baadaye kidogo nikaona mguu wa kaka ukitolewa na niliutambua kwa kuwa ulikuwa na kovu kwa nyuma,” alisema Issa.

Issa aliongeza kuwa baada ya hapo, alimpigia kaka yake simu ambayo ilikuwa haipatikani, na baadaye ikambidi arudi nyumbani huku akiogopa kumwambia mama yao na walipopiga simu ya shemeji yake ikapokewa na polisi na kuarifiwa kuwa anayepigiwa amekufa na yuko mochari.

Alisema siku moja kabla ya tukio, alikutana na kaka yake akitokea kwenye shughuli zake na alimsisitiza kukazania elimu kwa kuwa wakati mwingine alikuwa akimchangia ada na nauli ya shule.

Mdogo wa marehemu Zainab, Sharifa Ali, alisema siku moja kabla ya tukio, dada yake alimpigia simu akimweleza kuwa angekwenda kliniki na baada ya hapo angepitia kwa bibi yao Magomeni.

Alisema dada yake hakuwa na uchungu wa kujifungua na kwamba alikuwa akienda kwa ratiba za kawaida. Wawili hao walizikwa jana katika eneo hilo, katika makaburi matatu tofauti.

Katika hatua nyingine, eneo la Kibamba taarifa kuu iliyotawala midomoni mwa wakazi ilikuwa msiba huo ambapo asilimia kubwa ilikuwa ya wakazi wa pale, hali iliyowafanya kutafakari wahudhurie msiba upi.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya abiria wote 11 waliokuwa katika Toyota Hiace namba T615 AJW ikitokea Kibamba kwenda Ubungo ambapo iligongana na lori la mafuta ya taa aina ya IVECO Fiat namba T189 ABP na tela lake namba T192 ABP.
Hadi jana asubuhi watu watano walishatambuliwa.Imeandikwa na Lucy Lyatuu; SOURCE:HABARI LEO

Jk azindua kitabua cha historia ya harakati za Sir George


JK akiwa katika picha ya pamoja na Joseph Kahama(Wanne kushoto) ambaye ni Mwandishi wa kitabu kinachohusu maisha ya mwanasiasa mkongwe Sir.George Kahama wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho uliofanyika jijini Dar. Wengine katika picha kutoka kushoto ni Rais Mstaafu awamu ya Tatu Benjamim Mkapa, Sir Geroge Kahama(wapili kushoto) na kulia ni Rais Mstaafyu awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi. Picha na mdau Freddy Maro wa Ikulu

JK akikata akizindua kitabu kinachohusu historia ya maisha ya utumishi serikalini ya Mwanasiasa mkongwe Sir.George Kahama wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho uliofanyika katika viwanja vya ikulu jijini Dar usiku wa kuamkia leo. Kutoka kushoto waoshuhudia uzinduzi huo ni Rais Mstaafu awamu ya tatu Benjamin William Mkapa, Mwanasiasa mkongwe Sir.George Kahama(wapili kushoto), Rais Mstaafu awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi(wanne kushoto) na watano kushoto ni Mwandishi wa kitabu hicho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Royalty Bwana Joseph kahama

Friday, March 26, 2010

Mamia ya miti yapandikizwa Dar




Mkurugenzi Mtendaji wa Zain Tanzania Khaled Muhtadi (kushoto) akipanda mti kuazimisha siku ya utunzaji wa mazingira jana jijini Dar es Salaam. Kampeni hiyo imeendeshwa na Shirika la linalojishugulisha na shuguli za utunzaji wa mazingira na mimea la WWF kwa kushirikiana na Zain Tanzania. Kulia ni Meneja Uhusiano wa Zain Tanzania Muganyizi Mutta.

======================================

MAMIA ya miti imepandwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam katika zoezi lililofanywa na kampuni ya simu za mikononi nchini Zain Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Mazingira na Mali hai zingine (WWF) pamoja na Manispaa ya Kinondoni jana walishiriki kazi ya upandaji miti, ili kushiriki saa moja ya kuzima taa katika miji mikubwa duniani.

Saa moja ya kuzima taa huadhimishwa Machi 27 ya kila mwaka kwa nia ya kuonyesha umuhimu wa kupunguza hewa ya ukaa na uhifadhi wa mazingira na kutoa elimu juu ya athari ya uharibifu wa mazingira kwa binadamu.

“Kampeni hii ilianza rasmi mwaka 2007 nchini Australia hadi sasa ikiwa inatarajia kupata nchi washiriki zaidi ya 120 ukilinganisha na miji 88 iliyonga mkono suala hili hapo awali;

“Zoezi hili huenda sambamba na kuzima taa kwa muda wa saa nzima kuanzia saa 2.30 usiku tarehe 27 kila mwaka, hufanya hivi kwenye Miji mikubwa ili kuwakumbusha kuwa uhifadhi wa mazingira ni muhimu na kuna haja ya kupunguza joto duniani,”alisema Meneja uhifadhi wa WWF Tanzania Petro Masolwa.

Aliongeza kuwa, kulingana na hali halisi ya umeme Tanzania kuwa ya matatizo wao wameamua kufanya zoezi la upandaji miti badala ya kuzima taa, ili kuikumbusha jamii umuhimu wa kutunza mazingira.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Zain Tanzania Khaled Muhtadi alisema, wadau wa mazingira walioshiriki wameonyesha kuguswa na suala hilo na kuahidi kutoa ushirikiano pamoja na kampuni yake katika kutunza mazingira nchini.

“Tunafurahi kushiriki katika mradi huu, tunawashukuru wadau wa mazingira,Manispaa ya Kidondoni na WWF kuweza kufanya zoezi hili, tutatoa ushirikiano wa karibu ili kutunza mazingira,”alisema Muhtadi.

Mkuu wa Wilaya Kinondoni Jordan Rugimbana aliyasihi makampuni mengine kuiga mfano huo ili kuinusuru nchi kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kuna haja ya makampuni mengine kuiga mfano huo matokeo ya mafuriko kama yaliyoleta maafa Kilosa na ukame maeneo ya Loriondo ni mabadiliko yenye kuhitaji jitihada za maksudi kuchukuliwa ili kuinusuru nchi yetu,”alisema Rugimbana.

Miti hiyo aina ya Washington Palm ilipandwa katika manispaa ya Kinondoni kuanzia Moroko Mataa hadi Namanga, zoezi hilo likitarajiwa kuendelea katika sehemu nyingine za jiji la Dar es Salaam na nchi nzima. Imeandikwa na Aziza Athuman. SOURCE: MWANANCHI

Thursday, March 25, 2010

Ajali mbaya sana





Wananchi wakiwa wanaangalia ajali ya lori ainaya scania lenye namba za usajili T 169 ABF ambalo lilipata ajali baada ya kuligonga na kuliangukia toyaota Hiace yenye namba za usajili T615 AJW lililokuwalikotokea kibamab kuelekea Jijini Dar es Salaam,ambapo inasadikiwa watu zaidi ya kumi walikufa papo hapo.

Lori la mafuta likiwa linavutwa ilikiuweza kuondoa maiti ambazo zilkuwa zimelaliwa katika ajali hiyo

Lori likiwa linavutwa baada ya kupata ajli eneo la darajani Kibamba lenye nambari za usajli T 169 ABF (Picha zote na Sanjito Msafiri)

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&


TATIZO la kutokuwepo kwa vifaa vya ukoaji hapa nchini limeendelea kusababisha vifo vingi hasa ajali zinapotokea barabarani ambapo vinapohitajika hukosekana hivyo idadi kubwa ya watu kufa eneo la tukio .

Hilo limethibitika jana katika tukio la ajali lililotokea eneo la daraja la kibamba jirani kabisa na Mji wa Kibaha ambapo lori lililokuwa na shehena ya mafuta uzito wa lita 30,000 liliigonga gari aina ya Hiace na kuilalia kwa zaidi ya masaa 5 bila ya kuwepo kwa vifaa vya aina yoyote vya uokoaji.

Akizungumza katika eneo la ajali hiyo na waandishi wa habari Kamanda wa polisi kikosi cha usalama barabarani Kamanda Mohammed Mpinga alibainisha kuwa tatizo hilo lipo si kwa Jiji la Dar es salaam pekee bali ni la nchi nzima.

Alisema serikali kwa sasa ipo katika kuendeleza jitihada zake za uletaji wa kifaa cha uokoaji Break Down ,hata hivyo hajaweka bayana muda wa kuletwa kifaa hicho.

Ajali hiyo imehusisha lori hilo lenye namba za usajili T 189 ABD iliyokuwa na trela T 192 ABD iliyokuwa ikitokea Dar es salaam kuelekea Chalinze na Hiace T615 AJN iliyokuwa ikitokea Kibamba kwenda jijini Dar es salaam .

Tukio hilo limetokea majira ya saa 11 alfajiri jana na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 11 ambapo baadhi wametambulika kuwa ni Zainabu Ally ,Shukuru Hussein na Abuu Twaibu,na wengine waliotajwa kwa jina moja ambao ni Seif ambaye ni dereva wa Hiace, Bweto na Mama Peter wote wakiwa wakazi wa kibamba.

Katika eneo hilo ajali vilio vilitawala zaidi ya masaa manne kutokana na kila aliyefika eneo hilo kuona hali halisi ya ajali hiyo iliyokuwa ya kusikitisha kwani kila maiti iliyotolewa kwenye Hiace hiyo zilikuwa nyingine zikatika vichwa na kiwiliwili,utumbo nje.

Majira ya saa 4.30 ndipo break down lenye namba T 407 BDG na T 548 BDS kutoka kampuni binafsi ya Effco Crane iliyokodishwa kwa ajili ya uokoaji iliwasili eneo hilo na kuanza jitihada za kunyanyua lori na kutoa maiti zilizokuwemo ambazo hata hivyo hazikuweza kufahamika idadi kamili kwani zingine zilisagika midhili ya nyama buchani.

Hivyo kuwa kazi ngumu hata kwa Jeshi la polisi kupata idadi kamili ya waliokufa katika ajali hiyo mbaya.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo ilitokea wakati fuso la mchanga ambalo namba zake hazikuweza kupatikana ilipotaka kulipita gari jingine lililokuwa mbele na ghafla lilipoona gari jingine lilirudi katika sehemu ya awali hivyo lori kutaka kuigonga fuso na hivyo kutoka upande wa pili na kukutana na hiace na kuiburuza na kuzama nayo mtaroni na kusababisha ajali hiyo.

Polisi kutoka Dar es salaam waliweza kudhibiti hali ya usalama katika eneo la tukio ,kudhibiti wizi kutotokea,uhamishaji wa mafuta katika lori jingine kwa ajili ya kuepusha kulipa kwa moto kutokana na gari hilo kuwa na mafuta .

Hata hivyo polisi imesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambao madereva wengi hupelekea matatizo kama hayo kutokea,

Dereva wa lori ambaye anadaiwa kusababisha ajali hiyo amekimbia baada ya tukio na hadi sasa hajaweza kupatikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea. Taarifa ya Julieth Ngarabali, Kibamba.

Wednesday, March 24, 2010

Usafiri Dar es Salaam



Unaweza kufikiri kuwa tatizo la usafiri katika nchi yetu limepungua lakini halitaisha leo wala kesho hebu angalia hapa jiutihada zinazofanyika zimewezesha angalau watu wenye magari makubwa kama hivi kupunguza msongamano wa abiria lakini bado inatakiwa kuanzisha mabasi ambayo yatakuwa na jukumu la kuwabeba abiria wakati wa kwenda kazini na kurudi ili kupunguza msongamano wa vijiggari vingi barabarani.

Operesheni Sangara





Wakazi wa Kibaigwa Wilayani Kongwa mkoani Dodoma wakimlaki Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe kabla ya kuhutubia mkutano wa juzi, ikiwa ni sehemu ya ‘Operesheni Sangara’ inayoendelea mkoani humo. Picha na Jube Tranquilino.

habari ndo hiyo

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania, Ephraim Mafuru (katikati) akizungumza na waandishi wa habari wa HabariLeo na Daily News wakati Vodacom alipotembelea chumba cha habari cha magazeti hayo kutangaza rasmi pungozo la gharama za upigaji simu. Kushoto ni Mhariri Msaidizi wa Daily News, Gabby Mgaya na kulia ni Mkurugenzi wa Mahusiano wa Vodacom, Mwamvita Makamba.Punguzo hilo la gharama za upigaji siku linakwenda kwajina la HABARI NDIO HIYO.


Mkurugenzi wa Masoko wa Vodacom Tanzania Ephraim Mafuru(kushoto) Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd na kulia ni Mkurugenzi wa Mkuu wa Vodacom Foundation, Mwamvita Makamba wakizindua rasmi “habari ndiyo hii”kwa wateja wa mtandao wa Vodacom ambapo mtandao huo umeshusha gharama za maongezi kwa wateja wake kuongea kwa shilingi 1 kwa sekunde siku nzima kwa wateja wa Vodacom.

RAIS SAMIA AKUTANA NA WAZEE WA MIKOA YOTE NCHINI, AFUNGUA UKURASA MPYA WA MAZUNGUMZO YA KITAIFA

  Dodoma, Agosti 27, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na wazee wa Mkoa wa Dodoma pam...