Wednesday, August 20, 2025

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA TISA WA TICAD 9 NCHINI JAPAN









Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zinazoshiriki katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 9), unaofanyika nchini Japan kuanzia tarehe 20 Agosti 2025.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi leo kwa pamoja na viongozi wakuu wa dunia akiwemo Mheshimiwa Shigeru Ishiba, Waziri Mkuu wa Japan; Mheshimiwa João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU); Mheshimiwa António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN); Mheshimiwa Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC); Bw. Haoliang Xu, Kaimu Mkurugenzi na Naibu Msimamizi wa UNDP; pamoja na Bw. Makhtar Diop, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kwa niaba ya Rais wa Benki ya Dunia.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Japan, Shigeru Ishiba, ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya Japan na Bara la Afrika kupitia maeneo makuu matatu: uchumi, jamii, na ulinzi na usalama.

Kwa kuzingatia mahusiano ya muda mrefu na ya heshima kati ya Japan na Afrika, Waziri Mkuu ameweka msisitizo mahsusi katika:

  • Kutafuta suluhu ya changamoto za madeni yasiyohimilika kwa baadhi ya nchi za Afrika;

  • Kuimarisha mtangamano na mshikamano wa Bara la Afrika;

  • Kuwezesha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) kwa kuongeza ushirikiano wa kikanda;

  • Kukuza sekta binafsi ya Afrika kupitia ushirikiano wa moja kwa moja na sekta binafsi ya Japan;

  • Kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu, hususan vijana na wanawake, kwa kupitia programu za mafunzo, ubunifu na startups;

  • Kuunga mkono juhudi za Afrika katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote.

Kwa upande wake, Tanzania inaendelea kuthamini na kushirikiana na Japan katika kuimarisha maendeleo endelevu na kukuza ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii, kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Bara la Afrika kwa ujumla.

No comments:

KASI NDOGO YA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA CHALINZE- DODOMA YAMKASIRISHA DKT. BITEKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka ...