Monday, August 04, 2025

BALOZI CHANA ASHIRIKI URITHISHAJI KWA VITENDO KATIKA MAONESHO YA NANENANE







Dodoma, Agosti 4, 2025
– Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Balozi Pindi Chana, amefanya ziara maalum katika banda la Makumbusho ya Taifa lililoko kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma. 

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Wizara kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini yake, hususan katika maeneo ya urithishaji wa historia, utamaduni na sayansi ya Taifa kwa umma.

Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri alipokelewa na maafisa waandamizi wa Makumbusho ya Taifa waliomueleza kwa kina kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuhifadhi, kutafiti na kuelimisha jamii juu ya urithi wa kihistoria na kitamaduni wa Tanzania. Alitembelea sehemu mbalimbali za banda hilo na kujionea namna taasisi hiyo inavyotumia teknolojia ya kisasa na mbinu shirikishi kufikisha taarifa muhimu kwa wananchi.

Mhe. Dkt. Balozi Chana alionesha kuridhishwa na juhudi za Makumbusho ya Taifa katika kushiriki kikamilifu kwenye Maonesho hayo, na alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ubunifu katika njia za kuwasilisha urithi wa Taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Alisema kuwa njia hizo zinapaswa kuwa na mvuto, hasa kwa vijana na wanafunzi, ili kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika kujifunza historia, mila na tamaduni za makabila mbalimbali ya Tanzania.

“Makumbusho ya Taifa yapo katika nafasi ya kipekee ya kuendeleza utalii wa ndani kupitia urithi wetu wa kihistoria na kitamaduni. Tunapaswa kuendelea kubuni mbinu mpya zitakazovutia vijana na kuwaelimisha kwa njia wanayoielewa,” alisema Mhe. Waziri.

Aidha, Mhe. Waziri aliwahimiza wadau wote wa sekta ya urithi na utalii kushirikiana katika kukuza maarifa ya kihistoria na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa.

Maonesho ya Nane Nane ni jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha huduma, teknolojia na mafanikio yao katika nyanja mbalimbali, likiwemo eneo la urithi wa Taifa. Banda la Makumbusho ya Taifa limeendelea kuvutia mamia ya wageni wanaojifunza historia ya Tanzania kupitia maonesho yaliyopangwa kwa ubunifu na weledi mkubwa

No comments:

Rais Samia Aongoza Kikao cha Kamati Kuu ya CCM Taifa Jijini Dodoma

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza kikao mu...