Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 6 Agosti 2025, amepokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Sudan nchini Tanzania, Mhe. Mohamed Abdalla Abdelhameed Ahmed, katika hafla rasmi iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Mara baada ya kuwasili, Balozi huyo alipokelewa kwa heshima zote za kidiplomasia na baadaye kukabidhi hati zake kwa Mhe. Rais Samia, ikiwa ni hatua rasmi inayomuidhinisha kuanza majukumu yake ya kidiplomasia hapa nchini.
Tukio hilo linafuata misingi na taratibu za kimataifa, ambapo Tanzania kama mwenyeji, inaonesha ukarimu, heshima na utayari wa kushirikiana na mataifa mengine katika masuala ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii.
Rais Samia alimtakia Balozi Mohamed Abdelhameed mafanikio mema katika jukumu lake jipya na kuahidi ushirikiano wa karibu kwa manufaa ya pande zote mbili.
Uhusiano kati ya Tanzania na Sudan umejengwa juu ya msingi wa heshima, mshikamano na ushirikiano wa kihistoria, na ujio wa balozi huyu mpya unaashiria mwendelezo wa kudumisha mahusiano hayo.
#IkuluYaChamwino #DiplomasiaTanzaniaSudan #RaisSamia #BaloziSudan
No comments:
Post a Comment