KONGWA – Viongozi wa kitaifa, wa kidini, pamoja na mamia ya wananchi wa Wilaya ya Kongwa na maeneo mengine nchini wamejitokeza kwa wingi leo, Agosti 11, 2025, kushiriki ibada maalumu ya kumuombea na kuaga mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Hayati Job Yustino Ndugai.
Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Michael, Dinari ya Kongwa, na kuongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dkt. Maimbo Mndolwa, akishirikiana na viongozi wa dini kutoka maeneo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Askofu Mkuu Dkt. Mndolwa ametoa salamu za faraja kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, akisisitiza kuwa mchango wa Hayati Ndugai katika kulitumikia taifa utaendelea kukumbukwa na vizazi vijavyo. "Mhe. Ndugai alikuwa kiongozi wa mfano, mnyenyekevu, na mwenye moyo wa kujitoa kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa Tanzania," alisema.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wakiwemo wabunge, mawaziri, viongozi wa vyama vya siasa, wakuu wa mikoa na wilaya, pamoja na wananchi wa kawaida waliofika kutoa heshima za mwisho. Uwanja wa kanisa ulijaa hadi kupindukia, ishara ya upendo na heshima kubwa ambayo Watanzania walikuwa nayo kwa marehemu.
Marehemu Job Ndugai, ambaye aliwahi kulitumikia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Spika kuanzia mwaka 2015 hadi 2022, alitambulika kwa uongozi thabiti, nidhamu ya kazi na kujali maslahi ya wananchi. Aidha, mchango wake katika maendeleo ya Wilaya ya Kongwa na taifa kwa ujumla umeacha alama isiyofutika.
Baada ya ibada, ratiba inaeleza kuwa mwili wa Hayati Ndugai utasafirishwa kuelekea nyumbani kwake kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho, ambapo viongozi mbalimbali na wananchi kutoka pembe zote za nchi wanatarajiwa kushiriki.
No comments:
Post a Comment