Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma leo, tarehe 26 Agosti 2025, ambapo alipokelewa kwa heshima kubwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama na Taasisi za Umma.
Ziara ya Makamu wa Rais mkoani humo inalenga kuimarisha jitihada za Serikali katika kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa magharibi mwa nchi.
Kesho, tarehe 27 Agosti 2025, Dkt. Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Tawi jipya la Benki ya CRDB katika Wilaya ya Buhigwe. Ufunguzi huo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kupanua huduma zake nchini, huku ukiendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza huduma za kifedha kwa wananchi wote, hususan waliopo vijijini na maeneo ya mipakani.
Wananchi wa Mkoa wa Kigoma na wilaya jirani wanatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa na upatikanaji wa huduma za kibenki, jambo litakalowezesha biashara ndogo, za kati na kubwa kukua, kuongeza fursa za ajira, na kuimarisha mzunguko wa fedha katika maeneo hayo.
Ziara hii pia inatarajiwa kutoa fursa kwa Makamu wa Rais kusikiliza na kujadiliana na wananchi kuhusu masuala ya maendeleo ya jamii, kilimo, biashara, na miundombinu, kwa lengo la kuendelea kuboresha ustawi wa wananchi wa Kigoma na taifa kwa ujumla.
#MakamuWaRais #PhilipMpango #Kigoma #CRDBBuhigwe #MaendeleoKwaWote #HudumaZaKifedha
No comments:
Post a Comment