Saturday, August 16, 2025

MAKAMU WA RAIS AONGOZA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC.










Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Tanzania katika Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ Troika) Jumuiya imejidhihirisha katika uimarishaji wa demokrasia na utawala bora.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ Troika Summit) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo nchini Madagascar.

Amesema katika kipindi hicho Tanzania iliunda na kuongoza Misheni nne za waangalizi wa Uchaguzi wa SADC kwa Nchi Wanachama zinazofanya chaguzi ambazo ni Jamhuri ya Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia. Ameongeza kwamba chaguzi hizo zilifanyika kwa amani na utulivu, kwa kuzingatia kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza chaguzi za kidemokrasia. Aidha amewashuruku wanachama wa SADC Organ Troika kwa msaada walitoa katika kuongoza Misheni hizo zilizokuwa na mafanikio.

Pia amesema jitihada zimefanyika katika kutafuta amani na utulivu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwemo kuunganisha michakato ya kutafuta amani ya Luanda Peace Process na Nairobi Peace Process kuwa mchakato mmoja kupitia vikao vya pamoja vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo ni kwa mara ya kwanza vimefanyika tangu kuanzishwa kwa SADC.

 Makamu wa Rais amesema pamoja na mipango mingine iliyopo inayolenga kukomesha changamoto za usalama Mashariki mwa DRC, ni lazima kuunganisha juhudi kwa kutumia mbinu za ndani ya Bara kwa kutoa uthibitisho wa kauli ya “suluhu za Kiafrika kwa matatizo ya Afrika” ikiwemo kujitolea muda na rasilimali katika mipango iliyoanzishwa ya kisiasa na kidiplomasia chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika (AU).

Makamu wa Rais amesema katika kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha usalama na amani katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni muhimu kuzingatia changamoto zinazojitokeza husuani ugaidi ambao usipodhibitiwa, una uwezo wa kusababisha madhara makubwa kwa Nchi Wanachama na eneo hilo kwa ujumla. 

Amesema ni muhimu kuimarisha Kituo cha Kukabiliana na Ugaidi cha Kanda (RCTC) ambacho kimeanzishwa ili kusimamia masuala yote yanayohusiana na ugaidi, ikiwa ni pamoja na utoaji wa mafunzo na upashanaji habari.

Makamu wa Rais amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, SADC bado inakabiliwa na changamoto za kiusalama ambazo zinazuia juhudi za kuwa na eneo lenye amani na utulivu. Amesema matukio kama uhamiaji haramu, ugaidi, ufisadi, migogoro ya ndani na usambazaji haramu wa silaha bado huathiri baadhi ya maeneo hivyo inahitajika msimamo wa pamoja katika kukabiliana na hali hiyo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema amani na usalama ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya Ushirikiano wa Kikanda uliopo. Ameongeza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshatekeleza wajibu wake na kuchukua hatua kubwa katika kuendeleza utimilifu wa malengo ya kikanda. 

Amesema Tanzania itaendeleza dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa karibu na Mwenyekiti wa Organ Troika anayekuja, Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Lazarus McCarthy Chakwera na Wajumbe wengine katika kuhakikisha utekelezaji kamili wa shughuli zilizokubaliwa na maamuzi juu ya kuimarisha amani na usalama ndani ya SADC.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameufahamisha Mkutano huo, kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya uchaguzi wake mkuu tarehe 29 Oktoba 2025. Amesema, Tume Huru ya Uchaguzi na wadau wa uchaguzi tayari wamefanya maandalizi yote muhimu ili kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa amani na wa kuaminika kwa mujibu wa vyombo vya sheria vilivyowekwa vya kitaifa na kikanda. Pia amealika Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC (SEOM) kupeleka Ujumbe wake wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao nchini Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi. Thabit Kombo amesema Tanzania imepokea pongezi nyingi kutoka kwa Mataifa ya SADC kutokana na uongozi wa mwaka mmoja wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ).

Amesema pongezi hizo zimetaja mafanikio mbalimbali kama vile kuikutanisha Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa mara ya kwanza kutafuta suluhu ya mgogoro Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Pia kufanyika kwa vikao vingi zaidi vya SADC Organ Troika vya Wakuu wa Nchi na Serikali, kutatua migororo ya Lesotho, Eswatin, Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji pamoja na migogoro midogo ya mipaka.

Amesema mafanikio mengine ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika SADC Organ Troika ni kuunganisha michakato miwili ya kuleta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Luanda Process na Nairobi Process) kuwa katika mwamvuli mmoja.

Katika Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) utakaofanyika kesho tarehe 17 Agosti 2025, Tanzania inatarajia kukabidhi uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ Troika) kwa Jamhuri ya Malawi.

No comments:

MAKAMU WA RAIS AONGOZA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Tanzania kat...