Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Januari 17, 2026 ameongoza kikao cha kazi cha ngazi ya juu kilicholenga kujadili ujenzi wa miradi ya barabara za haraka (Express Ways) kwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya usafiri nchini.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, kimewakutanisha viongozi wakuu wa Serikali na wataalamu wa masuala ya ubia, kwa lengo la kuweka mwelekeo wa pamoja kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa ya kimkakati itakayoboresha mtiririko wa usafiri, kupunguza msongamano na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Nchemba amesisitiza umuhimu wa miradi ya barabara za haraka katika kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Taifa, akieleza kuwa mfumo wa PPP unatoa fursa ya kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa kwa kushirikisha rasilimali, utaalamu na teknolojia kutoka sekta binafsi.
Amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi, huku ikihakikisha kuwa ubia unaoingia unaleta thamani halisi kwa Taifa.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, pamoja na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ambao kwa pamoja wameeleza dhamira ya Wizara zao kushirikiana katika kufanikisha miradi hiyo.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. James Kilabuko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, pamoja na watendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, David Kafulila.
Kwa mujibu wa maelezo ya kikao hicho, miradi ya barabara za haraka inayopangwa itakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha ufanisi wa usafiri wa abiria na mizigo, kuongeza usalama barabarani na kuvutia uwekezaji, sambamba na kupunguza gharama za usafirishaji.
Hatua ya Serikali kuimarisha matumizi ya mfumo wa PPP katika ujenzi wa miundombinu mikubwa inaonesha dhamira ya dhati ya kutafuta suluhisho bunifu na endelevu la kufanikisha miradi ya kimkakati, huku ikilinda maslahi ya Taifa na wananchi kwa ujumla.









No comments:
Post a Comment