Monday, January 12, 2026

TANZANIA INA FURSA KUBWA YA KUENDELEZA NISHATI YA JOTOARDHI; WAZIRI NDEJEMBI ALIELEZA BARAZA LA IRENA







📌Asisitiza ushirikiano wa taasisi za kifedha na Jumuiya za Kimataifa hasa katika hatua za utafiti

📌Akaribisha wawekezaji; Asema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya uwekezaji ikiwemo upatikanaji vibali na lesenii

📌Asema Tanzania ina maeneo 52 ya jotoardhi yenye uwezo wa kuzalisha megawati 5000

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema kutokana na uwepo wa vyanzo vingi vya nishati ya jotoardhi, Tanzania inayo fursa ya kuviendeleza vyanzo hivyo ili wananchi wapate nishati ya kutosha, nafuu na endelevu  ikiwa pia ni sehemu ya kuunga mkono malengo ya dunia ya kuelekea kwenye uzalishaji wa umeme unaotokana na nishati safi.

Akizungumza kwenye Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) katika Mkutano wa Mwaka wa Muungano wa Kimataifa wa Jotoardhi (Global Geothermal Alliance – GGA), unaofanyika Jijini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Waziri Ndejembi amesema  Serikali imeweka mipango ya uzalishaji wa umeme wa jotoardhi katika Dira ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) na Mkataba wa Nchi kuhusu Masuala ya Mabadiliko ya Tabia Nchi (NDCs).

Amesema Tanzania pia kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC) inaendeleza maeneo kadhaa ya kipaumbele ya jotoardhi ikiwemo Ngozi (MW 70), Songwe (MW 5–38), Kiejo-Mbaka (MW 60), Natron (MW 60) na Luhoi (MW 5), huku lengo likiwa ni kuwa na mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme wa megawati 130 ifikapo 2030 ambapo mtambo huo utaanza kwa kuzalisha megawati 30.

Katika Mkutano huo, Waziri Ndejembi amealika wawekezaji nchini akieleza kuwa Tanzania inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, kuimarisha mifumo ya kisheria na kanuni ili kutoa uhakika wa uwekezaji, kuboresha michakato ya kupata leseni na vibali pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa data za jotoardhi.

Aidha, ili kuweza kuiendeleza ipasavyo nishati ya jotoardhi Ndejembi amesema bado kunahitajika mikopo ya riba nafuu pamoja na kuwa na ushirikiano na Jumuiya za kimataifa pamoja na Sekta binafsi ili kukabiliana na changamoto ya uendelezaji hasa katika hatua za awali za utafiti ambazo zina gharama kubwa.

Ameongeza kuwa, Tanzania pia inakaribisha  mataifa yaliyopiga hatua katika uendelezaji wa jotoardhi kuendeleza Wataalam wazawa katika masuala ya Jotoardhi.

Ndejembi amesema kuwa kutokana na uwepo wa Bonde la Ufa, Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya jotoardhi vinavyoweza kuzalisha megawati 5,000 za umeme. Ametaja kuwa kuna maeneo 52 yenye viashiria vya jotoardhi ndani ya mikoa 16.

Akifungua mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IRENA, Gauri Singh amesema kuwa nishati ya jotoardhi ni muhimu duniani katika kutoa hakikisho la usalama wa nishati lakini ameeleza kuwa bado mchango wake bado ni mdogo duniani katika kuzalisha umeme hivyo vyanzo zaidi vinapaswa kuendelezwa.

Katika mkutano wa IRENA, Waziri Ndejembi ameambatana na Kaimu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bakari Ameir, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma pamoja na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Nishati

No comments:

TANZANIA INA FURSA KUBWA YA KUENDELEZA NISHATI YA JOTOARDHI; WAZIRI NDEJEMBI ALIELEZA BARAZA LA IRENA

📌Asisitiza ushirikiano wa taasisi za kifedha na Jumuiya za Kimataifa hasa katika hatua za utafiti 📌Akaribisha wawekezaji; Asema Serikali i...