Jengo la gorofa tisa linalomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF), maarufu kama Hifadhi House, lililopo eneo la Posta katikati ya Jiji la Dar es Salaam, limenusurika kuungua baada ya moto mkubwa kuzuka leo Januari 16, 2026, majira ya saa sita mchana.
Jengo hilo lililopo katika makutano ya Mitaa ya Azikiwe na Samora Machel, lilikumbwa na tukio hilo la moto katika mazingira ambayo chanzo chake bado hakijafahamika rasmi, hali iliyosababisha taharuki miongoni mwa wafanyakazi, wapita njia na wananchi waliokuwepo karibu na eneo la tukio.
Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dar es Salaam, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Frank Mwalongo, amesema kuwa Jeshi la Zimamoto lilipokea taarifa za dharura kuhusu tukio hilo majira ya saa sita na robo mchana, na mara moja vikosi vya zimamoto vilielekezwa eneo la tukio.
Mwalongo amesema kuwa kutokana na jitihada za haraka na ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, waliweza kuudhibiti moto huo kwa wakati, hatua iliyosaidia kuzuia jengo hilo kuungua na kuepusha uharibifu mkubwa wa mali.
“Tulifanikiwa kudhibiti moto kabla haujasambaa zaidi, hivyo kuokoa jengo pamoja na mali zilizokuwamo ndani yake,” amesema Mwalongo.
Ameongeza kuwa katika tukio hilo, watu wawili walijeruhiwa na waliokolewa salama kisha kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam (Mnazi Mmoja) kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Mwalongo, chanzo cha moto huo bado hakijabainika, na Jeshi la Zimamoto linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo na kuchukua hatua stahiki.
Kwa upande wao mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Rehema John na Jackson Emmanuel, wamesema kuwa moto ulianza katika sehemu ya chini ya jengo na kusambaa kuelekea juu, hali iliyosababisha hofu kubwa miongoni mwa watu waliokuwamo ndani ya jengo hilo, hususan waliokuwa kwenye gorofa za juu.
Mashuhuda hao wamekipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na vyombo vingine vya usalama kwa kufika kwa wakati na kuchukua hatua za haraka zilizosaidia kuwaokoa watu waliokuwamo ndani ya jengo hilo, pamoja na kudhibiti hali kabla haijawa mbaya zaidi.
Kwa sasa, hali katika eneo la tukio imerejea kuwa shwari huku uchunguzi ukiendelea, na mamlaka husika zikiendelea kutoa taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana.






No comments:
Post a Comment