Bodi ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB), inayofanya kazi chini ya Wizara ya Fedha, imetoa onyo kali kwa watahiniwa wote wa fani ya Ununuzi na Ugavi kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa kanuni na taratibu za mitihani, ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watakaobainika kufanya udanganyifu.
Onyo hilo limetolewa Januari 30, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Bw. Godfred Mbanyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu udahili na matokeo ya mitihani ya 32 ya bodi hiyo.
Bw. Mbanyi amesema adhabu kwa mujibu wa kanuni ni pamoja na kufutiwa matokeo ya mitihani yote, kusimamishwa kushiriki mitihani kwa mikao mitatu mfululizo, kutozwa faini au hata kifungo cha jela kulingana na uzito wa kosa.
Katika mitihani hiyo, jumla ya watahiniwa 1,291 walidahiliwa, ambapo watahiniwa 1,223 walifanya mitihani huku watahiniwa 68 wakikosa kushiriki kwa sababu mbalimbali.
Kati ya waliofanya mitihani, watahiniwa 595 sawa na asilimia 48.7 walifaulu, watahiniwa 589 (asilimia 48.2) wanarudia masomo yao, huku watahiniwa 39 sawa na asilimia 3.2 wakifeli na kuanza upya masomo yao katika ngazi husika.
Aidha, Bw. Mbanyi ameeleza kuwa watahiniwa wawili wa ngazi ya CPSP walikamatwa wakijihusisha na ukiukwaji wa taratibu za mitihani baada ya kubainika kuingia ndani ya vyumba vya mitihani wakiwa na karatasi zinazodhaniwa kuwa na majibu ya mitihani.
Amesema Bodi ya Wakurugenzi imeielekeza Kamati ya Usajili na Nidhamu kushughulikia suala hilo, na endapo wahusika watapatikana na hatia, watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa kanuni zilizopo.
Kwa sasa, matokeo ya watahiniwa hao yamezuiliwa na wahusika watapewa haki ya kusikilizwa mbele ya kamati husika.
Kwa upande mwingine, PSPTB imewahimiza watahiniwa waliokosa alama za kutosha kujisajili upya na kurudia masomo yao katika mitihani inayotarajiwa kufanyika Mei 2026.
Bw. Mbanyi pia amewakaribisha wahitimu wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi kujisajili kufanya mitihani ya kitaaluma ya PSPTB ili kupata sifa stahiki katika fani ya Ununuzi na Ugavi.
Kadhalika, wazazi, wadhamini na waajiri wametakiwa kuwasaidia watahiniwa kwa kuwalipia ada za maandalizi na mitihani, hatua itakayochochea ukuaji wa wataalamu wenye maarifa na ujuzi katika sekta hiyo muhimu.
PSPTB imetoa pongezi kwa watahiniwa wote waliofaulu katika ngazi mbalimbali, wakiwemo waliopata sifa za kutunukiwa Vyeti vya Professional Diploma, Graduate Professional na CPSP, pamoja na wahadhiri na wakufunzi kutoka vyuo na vituo vya mafunzo kwa mchango wao katika kuwajengea watahiniwa uwezo wa kufanya vyema




No comments:
Post a Comment